Tuesday, June 11, 2013

ASKARI POLISI WAFUKUZWA KWA AIBU NA KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA WIZI WA RISASI 1050

Na Thomas Dominick,
Musoma.

Jeshi la polisi mkoni Mara limewafukuza kazi kwa aibu na kuwafikisha Mahakamani askari wake wawili wanaodaiwa kukamatwa na risasi 1050 zinazodaiwa kuibwa kwenye kikosi cha kuzuia na kutuliza ghasia (FFU).

Askari ambao wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mara ni askari aliyekuwa na cheo cha sajenti Michael Reus wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoa wa Mara pamoja na askari mwenye cheo cha koplo Ally Machembe aliyekuwa akifanya kazi Kibaha mkoni Pwani.

Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, ilielezwa na mwendesha mashitaka wa Serikali Jonas Kaijage mnamo juni mosi mwaka huu majira ya saa ya usiku askari hao walikamatwa kwenye basi la Mohamed Trans linalofanya safari zake kati ya Musoma na Dar es salaam wakiwa katika harakati za kusafirisha risasi hizo.

Ilielezwa Mahakamani hapo kuwa watuhumiwa wanakabiliwa na makosa matatu ikiwemo kosa la kula njama za kufanya wizi, kosa la pili kumwibia mwajiri wao kwenye kambi ya FFU na kosa la tatu ni kukutwa na risasi 1050 zinazotumika kwenye bunduki ya SMG na SR pasipokuwa na kibali.

Watuhumiwa hao walipelekwa Mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambapo kila mmoja alitakiwa kuwa na dhamana ya shilingi milioni 5 na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali.

Kesi ya askari ambao awali walifikishwa katika Mahakama ya kijeshi na kufukuzwa kazi kutokana na kutenda makosa hayo,kesi inayowakabili imepangwa kusikilizwa tena Juni 24.

Naye kamanda wa Polisi Mkoa wa mara Absalom Mwakyoma alisema kuwa kutokana na kutenda kwa makosa hayo Jeshi hili liliwafikisha katika mahakama ya kijeshi na kuwatia hatiani ambapo wote wawili wamefukuzwa kazi kasha kupelekwa mahakama ya kiraia.

“Tumewafukuza kwa aibu kutokana na makosa yao hayo ya kulidhalilisha jeshi letu kwani hatupo tayari kuona makosa kama hayo yakiendelea ambayo yanahatarisha usalama wa wananchi,”alisema Mwakyoma.

Inadaiwa askari huyo wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) Mkoani Mara alikuwa katika Ghala la kuhifadhia silaha huenda alikuwa akijihusisha na biashara za kuuza silaha hali iliyopelekea kuwekwa kwa mtego huo ambao ulifanikiwa kumkamata.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment