Saturday, June 15, 2013

MHUDUMU ATAKAYE UZA DAMU KWA MGONJWA ANAYEHITAJI DAMU KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA PAMOJA KUFUKUZWA KAZI.

 Mhudumu wa Damu salama akimchoma sindano kwa ajili ya kutoa damu Mwandishi wa Blog hii Thomas Dominick siku ya Maadhimisho ya Damu salama kitaifa ilifanyika Manispaa ya Musoma.
 Mwandishi wa habari wa Blog hii akitoa damu katika maadhimisho ya Damu salama Duniani ambapo kitaifa ilifanyika Manispaa ya Musoma Mkoani Mara.
 Naibu Waziri wa afya na Ustawi wa jamii Dkt. Seif Rashid akipata maelekezo toka kwa wahudumu wa Damu salama katika viwanja vya shule ya Msingi Mukendo Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara.
 Viongozi wa siasa waacha itikadi zao wamejumuika katika maadhimisho ya Damu Salama Mwenye suti ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime John Henjewele, kushoto kwake ni Katibu wa CCm Wilaya ya Musoma Musa matoroka, na kulia kwake ni Christant Nyakitita Mwenyekiti wa Mkoa Chama cha DP na wa mwisho ni Elisha Erasto Katibu wa Mkoa wa chama UDP
 Dkt. Seif Rashid mwenye miwani akiangalia wacheza ngoma hawapo pichani siku ya maadhimisho ya Damu salama Duniani yaliyofanyika kitaifa Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara.
Mwakilishi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Mkoa wa Mara, Emannuel Amas akipokea cheti maalumu kutoka kwa mgeni Rasmi  Dkt. Seif Rashid ikiwa kutambua mchango wa Televisheni katika kuhamasisha uchangiaji damu kwa hiari.



* Manispaa ya Musoma yavunja rekodi kwa kuchangia

*Vyombo vya habari vyatakiwa kuendelea kuhamasisha



Na Thomas Dominick,
Musoma
SERIKALI imesema kuwa haitasita kumchukulia hatua za kisheria pamoja na kumfukuza kazi mganga, muuguzi na mhudumu yeyote wa afya ambaye atabainika kuuza damu kwa mgonjwa anayehitaji damu.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dokta Seif Rashid katika maadhimisho ya siku ya uchangiaji damu Duniani ambapo kitaifa ilifanyika Manispaa ya Musoma Mkoani Mara.

Katika takwimu za awali jumla ya chupa 5479 katika wilaya za mkoa huo zilikuwa zimeshachangiwa ambapo lengo lilikuwa kila wilaya ichangie chupa 600 ambapo zingekusanywa chupa 3600 lakini lengo hilo limevukwa.

Wakati zoezi la kuchangia likiendelea katika viwanja vya shule ya msingi Mkukendo manispaa ya Musoma ambapo ilidaiwa kuwa Manispaa ya Musoma iliongoza kwa kuchanfi chupa 1230, Tarime 1078, Butiama, 954, Rorya 874, Bunda 695 na Serengeti 648.

“Kwanza napenda kutoa wito kwa waganga, wauguzi na mhudumu yeyote wa afya ambaye atabainika kuuza damu kwa wagojwa ambao wanahitaji damu kuwa tukithibitisha kuwa ameshiriki kitendo hicho tutamchukulia hatua za kinidhamu pamoja na kumfukuza kazi,”alisema Dkt. Seif.

Katika hatua hiyo Dokta Seif aliwahamasisha wananchi  nchini kujitokeza kwa wingi kuchangia damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya watanzania wenzao, hivyo wajitokeze katika vituo vya mpango wa Taifa wa damu salama au hospitali zilizo karibu.

“Kuchangia damu mara kwa mara kutasaidia kuwa na akiba ya damu ya kutosha hivyo kusaidia kupunguza kupunguza vifo ambavyo vinaweza kutokea kwa wagonjwa wanaohitaji damu kwa sababu ya ukosefu wa damu hospitalini,”alisema.

Alisema kuwa mikakati mbalimbali imewekwa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto na kufikia malengo yake kwa kufanya kampeni ya uhamasishaji uchangiaji damu kwa hiari katika jamii.

Kuweka mikakati ya kujua matumizi halisi ya damu nchini na kuwakumbusha madaktari, wauguzi na wataalam wa maabara juu ya matumizi sahihi ya damu na kuendelea kuelimisha jami kwa kutumia vyombo vya habari, vipeperushi na kutumia vifungashio vya damu vyenye ujumbe vya DAMU HAIUZWI.

Pia alisema kuwa wizara inatoa rai kwa waganga wakuu wa mikoa kwa kushirikiana na halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya huduma za damu salama ikiwemo ukusanyaji wa damu katika mikoa na wilaya.

Vile vile alitoa rai kwa vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na mpango wa Taifa damu salama katika kuhamasisha juu ya umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari ili wananchi amba wamekuwa na imani potofu kuhusu kuchangia damu, wabadili imani zao na tabia ili nao waanze kuchangia.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa alitoa maombi kwa wizara hiyo kushirkiana ili kupanua uwezo wa kupima na kuhifadhi damu musoma badala ya kituo cha kanda kilichopo Mkoani Mwanza.

“Sio kama wizara ihamishe kituo cha mwanza bali hii itasaidia kuinua hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ambayo wananchi wake watakapokuwa na mahitaji ya damu wasisubirie hadi kutoka mwanza,”alisema Tuppa.

Aliomba pia watoe adhabu stahili kwa kwa waganga, wauguz na wahudumu watakaobainika kuuuza damu kwa mgonjwa ambaye anahitaji damu ili kuokoa maisha yake.

Mwisho.
   

0 comments:

Post a Comment