Tuesday, June 11, 2013

AFISA MIPANGO MIJI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA RUSHWA MKOANI MARA

Na Thomas Dominick,
Musoma.

TAASISI ya Kuzuia na kupambana na rushwa Mkoani Mara imewafikisha mahakamani na kuwafungulia shauri la jinai namba 97 ya mwaka 2013 Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma kwa kupokea  rushwa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari inadaiwa Afisa mipango miji aliyefikishwa mahakamani hapo Richard Maganga kwa kosa la kupokea rushwa ya shilingi Milioni 3.7 na David Mtae ambaye ni mwakilishi wa Lipaz Consultants ya Dar es Salaam kwa kutoa rushwa kinyume na kifungu 15(1)(a) na 15 (1)(b) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya 2007.

Mashitaka hayo ya kudai,  kupokea na kutoa rushwa yamefikishwa
mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Ngigwana na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU wakili Mwema Mella.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa TAKUKURU Mkoa huo, Holle Makungu alieleza kwamba, afisa mipango huyo alipokea fedha hizo toka kwa mwakilishi wa kampuni hiyo inayojishughulisha na kutafuta maeneo ya vibali kwa ajili ya ujenzi wa minara ya simu.

Aidha Makungu alieleza kuwa mshitakiwa alipokea fedha hizo ili aweze kupitisha michoro na hatimaye kutoa vibali vya ujenzi wa minara hiyo vilivyokuwa vinaombwa kwa niaba ya kampuni ya AIRTEL na VODACOM.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Juni 25 mwaka huu na washitakiwa wote wawili wamerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni wadhamini wawili wa kuaminika ambao wanatakiwa kuwa na mkataba na mahakama wa shilingi Milioni tano kila mmoja.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment