Marehemu Daktari Joseph Nyamagirwa
Na Thomas Dominick
Musoma
DAKTARI Msaidizi Mkuu Daraja la kwanza wa Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Mara,Joseph Nyamagirwa (59)
amefariki Dunia juzi asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mkoa
wa Mwanza kwa tatizo la uvimbe sehemu ya chini ya utumbo mpana.
Daktari huyo ameacha pengo kubwa katika Hospitali ya Mkoa wa
Mara kutokana na kuwa tegemeo kubwa hasa kwa kutibu watoto na wanawake pamoja
na upasuaji ambapo kwa sasa hospitali hiyo inahitaji madaktari 12 na hivi sasa
waliopo ni watatu tu.
Akitoa taarifa ya kifo
hicho,Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Iragi
Ngerageza alisema kuwa Marehemu alikuwa na tatizo la tumbo ambalo alikuwa
akilalamikia kuwa linauma ambapo Jan.8 Mwaka huu alifika Hospitalini hapa kwa
matibabu ambayo iliwalazimu kumpeka katika hospitali ya Rufaa ya Bugando na
siku hiyo hiyo akifanyiwa upasuaji wa kina.
Alisema kuwa pamoja na jitihada za madaktari bingwa kuokoa
maisha yake lakini hali yake iliendelea kuzorota na hatimaye mauti kumfika Jan.
14 mwaka huu asubuhi ambapo alikuwa amelazwa katika chumba cha upasuaji idara
ya upasuaji (Surgical Department) chumba namba 6 C 607.
Alikielezea sifa za marehemu alisema kuwa ni Daktari pekee
ambaye alikuwa akifanya kazi kwa kujituma na kwa bidii kubwa na hata kama yuko
likizo ataitwa kufanya kazi atakuja haraka na kwa gharama zake kusaidia
wagonjwa ambao wanakuwa na hali mbaya.
“Kwa kweli Mkoa wa Mara tumepata pengo kubwa kumpoteza
ambapo marehemu aliitwa jina la utani la ‘Chief’kutokana na uchapakazi wake,alikuwa
alikifanya kazi ya uhakika kwa kuwa alikuwa atayari na uzoefu wa muda mrefu na
kila upasuaji unapofanyika lazima awepo akimabatana na jopo la madaktari
wengine kusaidiana nao na hatimaye kuokoa maisha ya wagonjwa wengi hasa akina
Mama Wajawazito na Watoto”Alisema Ngerageza.
Aidha ametoa wito kwa Wizara ya afya kuangalia uwezekano wa
kuleta madaktari kwani kuna upungufu mkubwa ambapo kwa upande wa madaktari
bigwa wanahitajika sita waliopo ni wawili tu na madaktari wasaidizi
wanahitajika 28 waliopo ni 16 wamebaki 15.
Akizungumzia elimu yake Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Mara,Faustin Bigambo alisema,alimaliza elimu ya Sekondari mwaka 1976 katika
Shule ya Sekondari ya Sengerema na kujiunga na Chuo cha Utabibu cha Tanga na
baadae kujiendeleza katika Chuo cha Madaktari wasaidizi cha Bugando
Mwanza(BMC).
Marehemu atazikwa Januari 17 mwaka huu kijijini kwao Butata
Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara,ambapo Maziko hayo yanatarajiwa kuhuduhuriwa na
viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,John Tuppa.