Thursday, March 28, 2013

MAUAJI YA KUTISHA MUSOMA KIKONGWE ANYONGWA




 *Wauaji wamfukia shambani kwake baada ya kumuua
 * Wananchi waitupia Serikali na Jeshi la Polisi Lawama
 * Wamkumbuka Kamanda Robert Boaz wataka arudishwe Mara



Ndugu wa Marehemu RoseMary Patrick (72) wakilia na kuomboleza baada ya kumpata akiwa ameuawa kwa kunyongwa kwa kutumia kanga yake na watu wasiojulikana akiwa shambani kwake na kumfukia katikati ya tuta la mihogo katika kijiji cha Bukanga Manispaa ya Musoma, Mkoa wa Mara.

                      
 Askari Polisi PC Regina akifungua kanga shingoni mwa mwili wa marehemu Rosemary Patrick iliyotumika kwa kumnyonga.

Bibi ambaye Jina lake halikupatikana mara moja alibebwa na wasamaria wema baada ya kupoteza fahamu wakati akiomboleza msiba wa ndugu yake Rosemary Patrick aliyeuawa kwa kunyongwa kwa kanga akiwa shambani kwake.
 
 Wananchi wa Kijiji cha Bukanga na maeneo ya jirani waliokusanyika katika shamba la marehemu kuona mauaji ya kinyama ya Bibi Rosemary Patrick (72) alieyeuawa kwa kunyongwa kwa kanga.


 Wananchi wa Kijiji cha Bukanga na maeneo ya jirani waliokusanyika wakiondoka baada ya Polisi kuchukua mwili wa marehemu Bibi Rosemary Patrick (72) alieyeuawa kwa kunyongwa kwa kanga.



 Wananchi wakishirikiana na Jeshi la Polisi kuubeba mwili wa marehemu Rosemary Patrick kutoka sehemu aliyenyongewa na kupelekwa kwenye gari la Polisi kwa ajili ya Kupelekwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa mara kwa ajili ya uchunguzi.






 Kaimu Mkuu  wa Upelelezi Wilaya ya Musoma Mjini Justine Shiganza akiuangalia mwili wa marehemu Rosemary Patrick aliyeuawa kwa kunyongwa kwa kanga yake kisha kufukiwa shambani kwake.

Na Thomas Dominick,
Musoma


BIBI mmoja aliyejulikana kwa jina la RoseMary Patrick (72) ameuawa kwa
kunyongwa kwa kutumia kanga yake na watu wasiojulikana akiwa shambani kwake na kumfukia katikati ya tuta la mihogo katika kijiji cha Bukanga Manispaa ya Musoma, Mkoa wa Mara.

Mwandishi wa blog hii alifika katika eneo la tukio na kushuhudia

tukio hilo na kuwatafuta ndugu wa marehemu kisha kufanya nao mahojiano juu ya mauaji hayo ya kutisha.

Tukio hilo ambalo lilitokea Machi 26 saa 12 asubuhi ambapo mume wa
marehamu Msira Masige (76) alisema kuwa mke wake huyo aliamka asubuhi siku ya tukio na  alikwenda kwa ajili ya palizi.

“Mke wangu aliamka asubuhi na kuniaga kisha kuelekea shambani lakini
mpaka inafika majira ya kurudi ambapo kawaida yake yake kurudi saa nne au tano asubuhi, lakini haikuwa hivyo ndipo tulipoamua kwenda shambani kumtafuta bila mafanikio,”alisema Masige.

Alisema kuwa baada ya juhudi za kumtafuta huku na kule walirudisha
juhudi katika maeneo mbalimbali ya shamba hilo ndipo walipobaini kuwa ameuawa na kufukiwa katikati ya tuta la shamba la mihogo.

“Tulirudi tena shambani kwa ajili ya kuendelea kumtafuta na kundi la
wanakijiji wenzetu tukafanikiwa kumpata akiwa amaeuawa na kufukiwa kwenye tuta ndani ya shamba letu,”alisema

Pia mtoto wa marehemu Kulwa Msira (37) alisema kuwa wakati mama yake
huyo akiwa hajulikani alipo  watoto wake walikwenda shambani majira ya saa tatu asubuhi kulima na waliporudi waliulizwa kama wamemuona bibi yao na kujibu kuwa hawakumuona.

“Baada ya watoto wangu kujibu hivyo kwa kuwa kulikuwa na msiba Makoko
tukajua huenda alibadilisha nia na kwenda huko ndipo nilipoanza kupiga simu kila sehemu na kujibiwa kuwa hawajamuaona tukaanza jitihada za kumtafuta huku na kule,”alisema Msira.

Alisema kuwa baada ya kurudi shambani kwake waligundua kuna nyayo za
watu na mtu akiwa ameburuzwa wakafuatilia kisha kukuta mwili wa mama yao mzazi umefukiwa akiwa amesha kufa tayari.

Baada ya askari wa jeshi la polisi kufika eneo la tukio walifukua

mwili wa marehemu kasha kuupakia kwenye gari, ndipo Kaimu kamanda wa Upelelezi Wilaya ya Musoma Mjini Justine Shiganza aliwakusnya wananchi na kuzungumza nao jinsi ya kuweza kushirikiana na Polisi na kufanikisha kuwatia mbaroni wauaji hao.

“Ndugu zangu wa Bukanga poleni sna na msiba huu, lakini lengo la

kuwakusanya hapa ni kutaka kusaidiana jinsi ya kuweza kuwapata wauaji ambao wanaendeleza mauaji katika maeneo yetu kwa kuwa ninyi ndio mnaoishi nao na tunachohitaji wote ni kukomesha matukio haya ya kutisha,”alisema Shiganza.

Alisema kuwa kama kuna mtu ambaye anajua kuna mtu alikuwa na kisasi na
familia hiyo atoe taarifa polisi na kasha yeye mwenyewe aliwapatia namba yake ya simu ya mkononi kwa ajili ya mawasiliano zaidi na kufanikisha kuwakamata wauaji hao.

Baada ya Shiganza kumalizakuongea wananchi walipaza sauti zao na
kulaumu jeshi la Polisi na Serikali kushindwa kuzuia na kukomesha matukio hayo ya kikatili wanayofanyiwa wananchi wa Mkoa huo.

“Matukio haya ya kutisha sasa yamekuwa ya kawaida kwa mkoa wetu hasa
wilaya mbili za Butiama na Musoma Mjini, Serikali na Jeshi la Polisi limekaa kimya kabisa na tumaini wanafurahia kuoana wananchi wao wanauawa ovyo,”alisema Manyonyi Emanueli Mkazi wa kijiji hicho.

Mkazi mwingine wa Kijiji jirani cha Mahare aliyejitambulisha kuwa

Mwenyekiti wa kijiji hicho, John Magesa alisema kuwa mauaji ni tatizo sugu kwa wakazi wa wilaya hizo mbili ambayo inahitaji njia mbadala ya kulipatia ufumbuzi wa kudumu.

“Wauaji wanafanya wanavyopenda tena bila wasiwasi kwa uhuru zaidi
serikali inataka tufanye ulinzi shirikishi nyakati za usiku na wauaji wanafanya matukio yao kuanzia asubuhi, kuna watu wanaonekana wanawinda kwa mbwa na manati lakini ndio wauaji wenyewe hao kinachotakiwa serikali ya wilaya ifanye vikao na serikali za vijiji kuona ni jinsi gani itawalinda wananchi wake,’alisema Magesa.

Wananchi hao hawakusita kusema kuwa Jeshi la polisi kwa sasa halifanyi
kazi yao ipasavyo na matukio hayo yamekuwa mengi baada ya Kamanda wa Polisi Robert Boaz kuhamishiwa Mkoa wa Kilimanjaro ambaye aliunda vikosi kazi vilivyofanya kazi usiku na mchana na kuvisimamia ipasavyo pamoja na kutumia kikamilifu dhana ya Polisi jamii na matukio kama hayo hayakuwepo.

“Hatuji Kamanda wa sasa anafanya kazi gani Mkoani kwetu vikundi vyote
vilivyoundwa kaviua na kama vipo havina nguvu ndio maana wauaji wanapata nafasi ya kuua ndugu zetu Serikali kama inatusikia waturudishie aliyekuwepo mwanzo na huyu apelekwe sehemu nyingine ameshindwa kabisa kulinda maisha ya watu wa Mara,”alisema Kijana Emanuel Rhobi.

Pia waliomba katika matukio kama hayo mbwa wa polisi watumike ili
kubaini wauaji kwani muda mwingine baada ya kuua hufika maeneo hao kushuhudia kama wananchi wema ambapo mbwa hao wataweza kuwabaini walifanya kitendo hicho.

MWISHO.

0 comments:

Post a Comment