Friday, March 29, 2013

-Ijumaa Kuu : Kubusu Msalaba ni Kuabudu au Kuheshimu?

Na Thomas Dominick


LEO ni siku ya Ijumaa Kuu Wakristo nchini wanaungana na wakristo wenzao Duniani kote kwa kuadhimisha siku ya mateso ya Yesu Kristo Msalabani siku ambayo wanaitumia kama siku ya kumbukumbu ya mateso na kufa kwa mwokozi wao Bwana Yesu Kristo ambaye aliletwa na Mungu ili kuja kuukomboa ulimwengu uliojaa dhambi.

Ijumaa Kuu hutumika kwa maadhimisho ya mambo mengi sana ambayo wakristo wanayafanya katika siku hii pamoja na kufunga na kubusu msalaba ila Ijumaa Kuu hii tutakaloliangalia ni kuhusu msalaba kitendo cha kuubusu ni kuuabudu au kuuheshimu.

Ili tuweze kuelewa vizuri lazima tujue ibaba ni nini na kuna mambo gani yanahitajika katika ibada na kinachotusumbua wengi ni kushindwa kutofautisha kati ya ya kuheshimu na kuabudu.

Kwa maana hiyo maana ya Ibada ni utaratibu uliowekwa na kundi la watu kwa ajili ya kufanya sala na maombi kwa ajili ya kuabudu mbele ya yule anayeabudiwa na watu husika na huyo ndiye Mungu wa kweli mbele yao.

Utashangaa nikisema kuwa Mungu huyo anaweza kuwa jua, jiwe, mti au chochote kile kilichoandaliwa na watu husika jambo kubwa nikuhakikisha shida zao zinapokelewa na kufanyiwa kazi na kujibiwa kama walivyotarajia.

Kwa hiyo penye ibada pana mungu yaani kile kinachoabudiwa na ili ikamilike na kuitwa ibada kuna mambo saba yanahitajika navyo ni Kuheshimu, kutukuza, kuabudu, kutoa sadaka, kusujudu, kusifu na kushukuru.


Kubusu.

Neno Kubusu lina maana nyingi tofauti kutokana na kila Taifa likiwa na tafsiri yake lakini kuabudu ni ishara au dalili ya upendo, Heshima na Furaha.

Biblia inatuambia kuwa hata wakristo wameagizwa wasalimiane kwa busu takatifu (2 Wakorintho 13:12) na tunaona viongozi mbalimbali wanapokutana wanakumbatiana na kubusiana kadhalika hata wazazi huwabusu watoto wao wachanga ili kuwafurahisha.


Kuabudu.

Neno kuabudu maana yake kuwa mtu au watu wanakisujudia au kukitukuza kitu fulani na kupeleka shida zao na kwa madai kuwa watapona au kupata faraja kutoka pale wanapozipeleka shida zao kwa yule wanayemuabudu na kutegemea kuwa matatizo yao yataisha kupitia kwake.

Mfano kila mmoja duniani anamuabudu yule anayedhani ni Mungu na Mitume wake kutokana na imani za kila mtu kwa kupelekea shida zake kwa njia mbalimbali na kujua yeye pekee ndiye atakayemsaidia katika matatizo yake.


Kuheshimu.

Heshima inayozungumzwa katika makala hii ni ile ya kujishusha na kumwinua Mungu. si heshima ya juu juu tu, bali ni heshima yaenye 'ADHAMA'. Ndani yake kuna adhimisho. Adhama maana yake ni ukuu na enzi. Tunapomwadhimisha Mungu, tunaweka juu yake heshima, ukuu, mamlaka na utukufu kuwa ni yeye tu anayestahili kuwa navyo. (1 Nyakati 16:27, Mithali 8:18).


Je Kubusu Msalaba ni Ibada ya sanamu?

Inaonesha kuwa Mungu ndiye aliyekataza ibada ya sanamu na wakati huo huo Mungu alimuagiza Musa atengeneze sanamu ya nyoka wa shaba kule jangwani.


"Bwana akamwambia Musa, jifanyie nyoka wa shaba ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti. (Hesabu 21: 4-9)


Baada ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo inawafanya wakristo kujua kuwa Yesu ndiye nyoka wao wa shaba. Na ukimtazama yesu juu ya mti wa msalaba, utapona majeraha yako yote uliyotiwa na shetani. Yeye anakualika akisema;

"Niangalie mimi mkaokolewe, enyi nchi zote za dunia, maana mimi ni Mungu, hapana mwingine." (Isaya 45:22).


Pia Mtume Paulo naye anawaambia wakolosai kuwa,

"Basi vivifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uuasharati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu." (Wakolosai 3:5).


Kumbe, matendo maovu ndiyo namna ya kisasa ya ibada ya sanamu. Ni bure kuendelea kufikiri kuwa kubusu msalaba ni kuabudu sanamu. Wakristo lazima waelewe kinachosema.
Siku zote maadui wa ukristo wamekuwa wakijaribu kupotosha imani ya asili na kuleta mafundisho yenye kutia mashaka mioyoni mwa waumini. Wasipotambua hayo, watakuwa watu wa kuyumbishwa siku zote katika imani.


Ibada ya sanamu.
Tangu mwanzo Mungu alichukia sana ibada ya sanamu. wapinzani wa imani ya makanisa ya Kikatoliki na Kiapotoliki wanaitumia sababu hii kupinga taswira ya msalaba.

Amri ya pili inasema hivi.

'Usijifanyie sanamu ya kuchonga wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini majani chini ya dunia, usivisujudie wala kuvitumikia....'(Kutoka 20:4-5).


Jambo la muhimu la kuangalia hapa ni kuwa, Mungu hakukataza kutengeneza sanamu. Maana maarifa ya watu wa zamani zile,utengenezaji sanamu ilikuwa ni sanaa ya kawaida kama vile sisi leo tunavyojivunia picha za kamera. katika amri hii Mungu anakataza; Kuvitumikia na Kuvisujudia.


Sanamu ya Yesu ina maana gani leo?

Hili ni swali muhimu sana. Lakini hebu tufikirie kidogo, kama kizazi chetu hiki cha leo kisingeona kumbukumbu ya picha ya Yesu msalabani, bila shaka wengi wasingejua jinsi ile Kristo alivyosulubiwa.

Basi Msalaba ni kielelezo, ni mfano tu, ni taswira ya kutufundisha hata twaweza kujua kwa urahisi jinsi ile mkombozi wetu alivyoangikwa juu ya mti wa ule wa msalaba. 


Kubusu msalaba kama tendo la ibada

Nimekwisha kusema hapo juu kuwa kuheshimu ni sehemu tu katika matendo saba yanayotafsiri ibada. Katika 'Misale ya Waumini' ya kanisa katoliki uk. 245 - 247, kubusu msalaba linaelezwa kama tendo la ibada. 

Nami sina ugomvi na jambo hilo. Maana sioni ubaya wowote endapo msalaba utaabudiwa. Kwa sababu msalaba umekuwa nyenzo muhimu sana katika kuukamilisha wokovu wetu. Pasipo msalaba hakuna wokovu.


Kwa nini Tunabusu msalaba.

Kama tulivyoona hapo juu kuwa busu ni upendo, heshima na furaha, basi kila Ijumaa Kuu tunaonyesha kwa vitendo jinsi tunavyompenda na kumheshimu mwokozi wetu Yesu Kristo kwa kubusu msalaba wake.

Maana ni katika huo ukombozi wetu unapatikana, wala si ajabu, kumbuka yule mwanamke aliyekuwa anatoka damu hakumgusa Yesu bali aligusa pindo la vazi lake tu na akapona na msiba wake (Marko 5:25-34).

Mtu wa Mungu wa kweli aliyekombolewa kweli hujiona mtupu kabisa anapofika mbele ya msalaba. Hii ni kutokana kwamba, kila aliyeokolewa ni kupitia msalaba tu. Ni hatari kuuukata msalaba, hiyo ni dalili ya wazi ya kupotea.

Mtume Paulo alipoongozwa na Roho Mtakatifu alipata kusema: 'Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tuliookolewa ni nguvu ya Mungu. (1 Wakorinto 1:18).

Unapobusu msalaba, kumbuka unataka kumwambia Bwana Yesu kuwa, 'Bwana asante kwa kazi yako iliyogharimu maisha yako ili mimi nipate uzima wa milele. Tena tunataka kufanana na mariamu, aliyebusu miguu ya mkombozi wake.(Luka 7:38)

Yaani, inaonesha unyenyekevu wetu kwake na kuikubali kwa moyo ile kazi kubwa asiyo na kifani aliyotutendea. Basi nataka ufahamu kuwa thamani ya msalaba ni ya juu mno kuliko vile ulivyokuwa unafikiri.


Je kuna Faida gani iliyopo kwa kubusu msalaba

Katika maandiko matakatifu inaonesha kuwa kuna faida nyingi sana kwa kuubusu msalaba maana umeponya wagonjwa. Kwa historia ya miaka hiyo tunaona Mt. Herena ndiye aliugundua msalaba wa Yesu huko Yerusalemu mnamo AD 326 baada ya kubomoa jingo na kuchambua ambapo alipata misalaba mingi lakini hakujua upi wa Yesu.

Ili waufahamu kuwa msalaba wa Yesu, Askofu wa Yerusalemu aliamuru aletwe mgonjwa akaugusa mmoja wa misalaba akapona wakajua kuwa ule ndio wenyewe. Msalaba huo uliheshimiwa sana hata ukawekwa katika kanisa kuu la Yerusalemu hadi AD 614 ambapo Waajemi waliuteka.

Lakini uliokolewa na Augusto Heraklio, na ulitekwa tena na Waislamu mwaka 636 AD hii inaonesha kuwa msalaba una faida nyingi kama ukiubusu au ukiushika.


Je msalaba unaweza kukubadilisha ufanane na Yesu

Msalaba ulimbadilisha Dismas yule haramia na kibaka mashuhuri na akashangilia wokovu siku ile ile.


Nguvu iliyomo katika Msalaba.

Tangu siku ya Ijumaa Kuu ya kwanza pale Golgotha, mpaka leo msalaba haujapoteza nguvu zake uliwaokoa wengi, leo upo kwa ajilii yako usiukimbie, ukaribie usiuonee haya ukumbatie usiuache, ubebe.


Piga alama yake tu kifuani mwako nao utakulinda wapo wanaoona kinyaa hata kupiga alama ya msalaba. Msalaba ni mlinzi wako hodari.

Nazungumzia nguvu iliyomo ndani ya msalaba kuwa una uwezo wa kufufua na ukifufuka hufi tena neno kuu kwa ajili yako leo ni uheshimu, upende, ufurahie msalaba maisha yako ya rohoni yatabadilika.


Shika sana ulichonacho

Tatizo kubwa linalolikumba kanisa kwa sasa ni wingi wa mafundisho na waalimu wanaotofautiana toka imani hata imani. Siku hizi kuna imani huria zinazotokana na dhana ya uhuru wa kuabudu.

Tulipofikia sasa si imani tena katika Roho Mtakatifu bali ni fujo na vurugu, hali ya unyenyekevu inapuuzika kila mmoja anataka afanye anavyoona machoni pake. yaani mtu akitofautiana na kiongozi wake hata katika mambo ya kawaida anajitenga na kuunda kanisa.

Wakristo wengi sasa wanajitenga na imani ya kweli na kujiunga na vikundi, walio wengi ni kwa kutokuelewa misingi mikuu ya imani yao ya asili ikiwemo ibada ya Juma Takatifu watu wametiwa mashaka juu ya usahihi wa imani yao.

Tunaona kuwa, sasa hivi tunaishi nyakati za mwisho zilizotabiriwa mvurugiko wa imani unaonekana kwa dhahiri yale waliyoyaacha mitume na mababa wa kanisa yanatiliwa shaka na kubezwa.
Tumechambua kwa undani tatizo la upotoshaji ninakuhamasisha na kukutia moyo kuwa si lazima nawe upotoshwe. Biblia inasema, 'Shika sana ulichonacho' (Ufunuo 3:11). 


Neno la mwisho

Tumekwishaona jinsi msalaba ulivyo mti wa muhimu katika maisha ya wakristo, mengi tumezungumza juu ya mti huo, wengine wamefundisha juu ya kufanya ishara ya msalaba katika vipaji vya nyuso zao. Hiyo yote ni kutaka kuonesha kuwa msalaba siyo kitu cha kawaida.

Kama ni mfuasi wa Kristo unacho cha kujivunia nao ni msalaba wa Yesu....! Waambie watu juu ya mti huo uzaao matunda yake kila siku usiojua kiangazi wala masika hata usiku wala mchanani wa ajabu sana unaookoa siku zote.

Basi wanapoutazama au kuubusu msalaba si kama wanauabudu bali ni kuonesha heshima na upendo wao juu ya mti ambao ni kielelezo cha mti uliotumika kuwakomboa watu wengi.

Kwa maana hiyo tulichojifunza kutoka katika makala hii kuwa wakristo hawaiabudu sanamu ya Yesu ila wanaiheshimu kwa kuwa ndani ya mioyo yao wanajua hakika ya kuwa hawaiabudu ile sanamu bali sanamu ile inabaki kuwa kielelezo tu.


Wao wanamwabudu Mungu tu na Yesu kristo mwana pekee wa mungu na Roho Mtakatifu katika umoja usiogawanyika wenye nafsi tatu.

Wakristo waliojaaliwa kuijua siri ya thamani iliyomo katika msalaba, waoneshe kwa vitendo heshima na upendo wao kwa kuubusu ni tendo la furaha, upendo na uondoe tashwishwi, hofu kwa kuwa tendo hilo ni safi tena ni takatifu na lenye heshima mbele za Mungu. 

MUNGU NA AKUTIE NGUVU ILI USIMAME KATIKA IMANI ILE ILE. 

Makala hii imeandaliwa kwa Msaada wa Bibilia na vitabu mbalimbali vya Kikristo Tanzania.
0716-000447 – 0767-000448

0 comments:

Post a Comment