Friday, March 29, 2013

WAKRISTO WA SASA TUNAJIFUNZA NINI KUTOKANA NA MANENO SABA ALIYOSEMA YESU MSALABANI SIKU YA IJUMAA KUU

YESU ATUNDIKWA MSALABANI AKIWA NA WAALIFU WAWILI
 YESU AUBEBA MSALABA WAKE KUELEKEA GOLGOTA KUSULIBIWA KWA AJILI YA DHAMBI ZA WANADAMU

Na Thomas Dominick
Musoma
Wayahudi walipomkamata Yesu walimtesa sana kuanzia usiku hadi asubuhi ya siku ya pili kisha alivishwa taji la miiba kichwani na mwanzi mkononi wake wa kuume pia wakati anapelekwa kusulubiwa alibebeshwa msalaba mzito ambao ulimuelemea.(Yohoha 27:29)

Alipofika sehemu iliyokuwa inaitwa golgatha yaani "Fuvu la kichwa" Yesu alivuliwa nguo zake na kumpigilia misumari mikononi na miguuni kisha kutundikwa msalabani.(Luka 15:22)

Padri John Mlekano wa Kanisa la Anglikana Tanzania anafafanua kiundani juu ya maneno saba ambayo Yesu Kristo aliyasema baada ya kutungikwa msalabani siku hiyo ya Ijumaa Kuu.

Pia anasema kuwa kwa maneno hayo wanadamu wanapaswa kuyatekeleza yale ambayo yanamlenga moja kwa moja sababu yanaweza kumsaidia katika maisha yake ya kidunia na kuishi katika maisha ya utakatifu.

Padri Mlekano anasema kuwa wakati Yesu ameangikwa msalaba alitoa jumbe mbalimbali ambapo alitoa maneno ya msamaha, usia, maneno ya maombi, maneno ya kuombea wengine, maneno ya maumivu yake mwenyewe.

"Maneno haya saba yalikuwa ni kauli zake za mwisho kabla hajakata roho ambapo katika maneno hayo saba hayakulenga kwa wanafunzi wake tu bali mengine yalikuwa kati yake na Mungu na hata yule mwalifu aliyeomba toba."alisema.


Neno la kwanza baba wasamehe maana hawajui watendalo (Luka 23:34)
Katika maneno haya yanawafundisha wanadamu wa leo kutoa msaamaha kwa mtu ambaye amekukosea na kukuudhi kwa namna yeyote ile lazima umsamehe kwa kuwa inawezekana hajui nini anakifanya kwa muda huo.

"Kwa maneno haya yanatugusa sisi moja kwa moja kutokana na dhambi zote tunazozifanya hapa ulimwenguni Mungu anakubali kutusamehe lakini baada ya kusamehewa tuna wajibu fulani wa kuutimiza kwake pamoja na kuomba toba."alisema. 

Alisema kuwa kwa somo hilo hapaswi mwanadamu kufanya makosa kwa makusudi kwa kuwa Mungu atamsamehe ila kama imetokea kwa bahati mbaya unatakiwa kufanya toba ya kweli na kutorudia tena kama yule mwalifu aliomba toba akiwa msalabani.


Amini nakuambia leo hii utakuwa nami mahala pema peponi 
 (Luka 23:43) 

Hapa Inaonyesha kuwa Yesu anatangaza ufalme wake katika, mazingira yale aliyoonekana kama mtu jambazi au mwalifu lakini wapo waliomuona kwa macho tofauti ya kuwa hakuwa mwalifu na hata mwalifu alikiri na kumuomba Yesu ampokee kule waendako.

Yule mwalifu alisema ‘EE Yesu nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako, na yesu akamwambia amini nakuambia leo leo hii utakuwa nami peponi.’(Luka 23:42-43) mwalifu yule aliyasema haya kwa kumtambua kuwa yeye ana mamlaka mbinguni hii inaonesha wote walikuwa na nafasi sawa ya kuomba msaamaha lakini mmoja alifanya kashifa na mwingine aliomba msaamaha. 

"Huu ni mfano wa kuigwa kwa maisha yetu ya leo maana inatuonesha yule aliyekashifu hakuona utukufu wa Mungu ila wa pili alisema kuwa sisi tunasitahili adhabu lakini huyu hakufanya kosa lolote na kitu cha kuigwa zaidi ni kutoka kwa yule mwalifu alifanya booking katika ufalme."alisema.

Aliongeza kuwa katika dunia hii wapo wanaoukataa ukuu wa Mungu ingawa upo katikati yetu na kutokubali kabisa kuutumia na wapo wanaouona na kuutumia.


Mama tazama mwanao mwana tazama mama (Yohana 19:26)

Huu ni usia ambao Yesu aliuacha kwa mwanafunzi wake na mama yake kwa sababu hapo alikuwa katika hali kama mwanadamu wa kawaida ambaye yupo katika hali ya kuondoka katika dunia hii anaacha mazingira ya namna gani huku nyuma kwa wanafunzi wake na mama yake.

"Alitambua kuwa wanafunzi wake walimtegemea yeye kwa kila jambo ila aliwaachia ujumbe huo unaowataka watunzane, mshikamane na wasimuangalie yeye kwa kipindi kile ambacho aondoka."alisema.

Lakini Yesu kwa neno hili anawataka wanadamu wasikate tamaa maana watu wengi wanapoondokewa na wale watu muhimu katika maisha yao wanakata tamaa kabisa ila yeye anawataka waendelee kwa jinsi ile alivyokuwa alipowaacha hadi siku ambayo wanadamu wote watakapokutana nao katika ufalme wake.


Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha (Mathayo 27:46)

Katika maneno haya tunapata fundisho kabla Yesu hajasulibiwa msalabani tulimbebesha mzigo mkubwa wa dhambi zetu kama kafara ateswe na wanadamu wapate kupona.

"Aliwekwa msalabani kama mwalifu, mtenda dhambi ama mtu wa kawaida lakini kiumungu alichukua uovu wetu wote na kwa namna hiyo hakuwa karibu na Mungu katika hali ile anausikia ule uchungu wa kibinadamu."alisema.

"Kwa sababu sisi wakristo tunaamini yesu alikuwa Mungu asilimia mia na mwanadamu asilimia mia kitu ambacho ni kigumu kidogo kwa kumueleza kwa mtu asiyekuwa mkristo haya ni mambo ya imani."aliongeza.

Hivyo katika mazingira yale pale msalabani Yesu hana uungu huwezi kusema kwamba mungu amesulibiwa aliyesulibiwa pale ni Yesu katika nafsi yake ya uanadamu yaani mwanadamu kwa asilimia mia kama unavyojua katika mazingira kama hayo mtu kukosa msaada katika mazingira magumu kama yale lazima ulalamike.

Kwa Hali hii Yesu anamlilia Mungu hili ni ombi lake yeye na Mungu ya kwamba anajisikia yupo mpweke anamlalamikia Mungu kwa nini amemuacha wakati kipindi chote alikuwa karibu naye. 

"Sasa basi fundisho linakuja kwetu sisi kuwa ukipatwa na shida usikimbilie kwenye njia ya mkato kama vile kwenda kwa waganga wa kienyeji au kumtegemea mwanadamu mwenzako kwa jambo ambalo mungu pekee ndiye anayetakiwa kupelekewa shida zako zote, tujue kuwa tuna mtetezi wetu ni Yesu ambaye anaweza kumaliza shida zetu."alisema.

Alisema kuwa kama umeumizwa katika jambo fulani mpigie Mungu magoti umweleze shida yako pale, usiende kuagua, usikimbilie kutoa au kupokea rushwa au kuiba na kusema nina njaa sasa ngoja nikaibe au mbona watoto wamefukuza shule ngoja nikafanye ukahaba nipate hela ya chapu chapu.

"Tusiende kwenye dhambi ila tukimbilie kwanza kwa Mungu tukiwa katika furaha ama katika huzuni yeye ndiye wa kumlilia hicho ndicho tunachojifunza kutoka katika neno hili."alisema.

"Bwana Yesu pale hakulalamika kuwa Mfalme Kaisari mbona mimi nateswa hapa au Pilato kwa nini umeruhusu nisulibiwe au wanafunzi mbona mmeniacha hakuzungumza habari yeyote iliyoonyesha kuwa anamtegemea mwanadamu lakini alionesha kuwa katika shida yake Mungu ndiye aliyekuwa mbele yake na anayeweza kumsaidia katika mateso yake."alifafanua.


Naona Kiu (Yohana 19:28)
"Kiu hii aliyoiona ni kutokana na hali ya uchovu tukumbuke pale yupo katika nafsi ya binadamu na ameteswa usiku kucha tangu jana jioni amepita akiburuzwa na mchana wote jua, msalaba, viboko na miiba lazima atajisikia kiu."alisema. 

Aliongeza kuwa "hapa kuna namna mbili ya kiu ile ya maumivu ya kimwili ambao sasa anasikia mwili unahitaji maji na kiu nyingine inayotafsiriwa kiroho ni kiu ya kuwa na hamu ya kuukomboa ulimwengu nina kiu na hawa watu kwamba wote wangejua kilichonifanya mimi kuja duniani ni kwa ajili yao ninapoondoka watakuwa pamoja nami au watapotea tena."alisema. 


Imekwisha (Yohana 19:30)

Neno hili alilisema baada wale askari kumpelekea chombo chenye siki ili anywe na amalize ile kiu aliyokuwa anaiona lakini baada ya kuipokea alisema kuwa Imekwisha ni neno tu la kukataa kuwa siki yenu sina haja nayo ila kile kilichokuwa rohoni na kilichonileta hapa Duniani nimekimaliza. 

"Fundisho tunalipata ni kuwa baada ya kazi mzito iliyokuwa imemleta Yesu katika ulimwengu huu ameimaliza sasa kazi iliyobaki kwetu wanadamu ni kushika imani na kumkiri kuwa ndiye mwokozi wetu na tukifanya hivyo tutakuwa tumefungua milango yote ya mbinguni na kuingia na kuishi huko kwa raha."alisema.


Baba mikononi mwako naiweka roho yako (Luka 23:46)

Baada ya kufanya kazi ngumu duniani ya kuwatafuta na kuwakomboa wanadamu na kupelekwa msalabani na kuona ametimiza kile alichotumwa na baba yake anasalimisha roho yake kwa kuiondoa ili apumzike na kuikabidhi kwa baba yake.

                       
"Hili nalo ni somo ambalo tunafundishwa kuwa kabla hatujalala tuwe na desturi ya kupiga magoti na kumwambia Mungu kuwa sasa naingia katika hali ya kutojitambua roho yangu hii naikabidhi mikononi mwako usipoamka ipo salama na ukiamuka nayo ipo salama."alisema.

Padri Mlakano anasema kuwa kutokana na somo hilo watu wajenga tabia ya kufanya sala kabla ya kulala, tujue kuna mtu mwenyewe ambaye anamiliki vitu vyote na kila kitu ni chake ina maana kama ukifa hiyo roho haifi inarudi kwa aliyeileta mwili unakwenda kutupwa, roho ni kitu cha thamani ambacho muda wote kinatakiwa kuwa katika hali ya uangalizi wa mwenye chake (Mungu). 

"Hapa utagundua miili yetu ni kama bagi maana wewe ukisafiri nguo zako unazifua na kuweka katika bagi na kwenye gari wanaweza kuliweka kwenye buti lakini mwisho wa safari yako unachojali ni nguo zako zipo salama. Ina maana hii miili ni kasha tu ambapo Mungu ameweka kilicho chake ambayo ni roho."alisema.

Padri Mlekano anamaliza kwa kusema kuwa yote tuliojifunza katika maneno saba aliyosema Yesu msalabani kuwa yote ni mafundisho ya namna fulani ambapo ujumbe wake unaweza kuupokea.

Lakini sio kama maagizo au amri kuwa tuyafuate bali ni vielelezo tu na ujumbe na kwamba kama utausikia utajua namna gani utaenenda katika ulimwengu huu uliojaa kila aina ya dhambi.

MUNGU AKUBARIKI UDUMU KATIKA NENO LAKE MILELE AMINA
0716 000447 / 0767 000448

0 comments:

Post a Comment