Wednesday, April 10, 2013

ANGLIKANA YAKABIDHI MSAADA WA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA BILIONI 1.041


    

     * Wahisani wataka watanzania kuwaamini madaktari wao
     *  Askofu Hilkiah Omindo asema kanisa lipo kwa ajili ya Jamii
     * Wassira asema maendeleo hayaji kama mvua


 Wananchi wa Wilaya ya Bunda wanachungulia madirishani jengo jipya la Upasuaji ambalo lina vifaa tiba vya kisasa vya upasuaji vilivyokabidhiwa hivi karibuni na Kanisa la Anglikana Tanzania Jimbo wa Mara kwa kushirikiana na  Serikali ya Italia kupitia shirika la ARCS
 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Christopher Sanya akiangalia kwa makini vifaa tiba vya upasuaji katika Hospitali Mpya ya Wilaya Bunda.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira akipokea maelezo ya utendaji wa kazi wa vifaa tiba vya upasuaji ukiwa ni msaada toka  Kanisa la Anglikana Tanzania Jimbo wa Mara kwa kushirikiana na  Serikali ya Italia kupitia shirika la ARCS
Hiki ni chumba kimojawapo ambacho Vifaa tiba vya upasuaji vimeweka na hii ni moja ya mashine kwa ajili ya upasuaji msaada toka Kanisa la Anglikana Tanzania Jimbo wa Mara kwa kushirikiana na  Serikali ya Italia kupitia shirika la ARCS

 Hii ni sehemu ya upasuaji kama inavyoonekana katika hospitali mpya ya Wilaya ya Bunda Kanisa la Anglikana Tanzania Jimbo wa Mara kwa kushirikiana na  Serikali ya Italia kupitia shirika la ARCS


Na Thomas Dominick,
Bunda

KANISA la Anglikana Tanzania, Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Serikali ya Italia kupitia shirika la ARCS imezindua na kukabidhi jengo la upasuaji na vifaa tiba na upasuaji vyenye jumla ya shilingi Bilioni 1.041 katika Hospitali mpya ya Wilaya ya Bunda iliyopo katika eneo la Manyamanyama, Mkoani humo.

Akisoma taarifa fupi wakati wa uzinduzi na makabidhiano hayo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, Mratibu wa afya na mratibu  wa CBR Dayosisi ya Mara Dkt. Henry Yoggo alisema kuwa fedha hizo zil;itolewa na wafadhili hao pamoja na Halmashauri ya Bunda na Kanisa hilo.

“Hadi mradi huu unafikia hatua hii tumeshatumia jumla ya shilingi Bilioni 1.041 ikiwa ni gharama za vifaa tiba na vya upasuaji uliogharimu shilingi milioni 313 na shughuli zingine za mradi pia umegharimu milioni 121 na sehemu iliyobaki katika gharama iliyotajwa hapo juu imetokana na nguvu ya kujitolea,”alisema Dkt. Yoggo.

Alisema kuwa kukamilika kwa Hospitali hiyo itatoa huduma mbalimbali iliwepo na utoaji wa huduma ya afya ikiwa pamoja na kufanya upasuaji, kuanzisha huduma ya kliniki ya kupima kansa ya shingo ya kizazi kwa akina mama, kuendesha mafunzo kwa watumishi mbalimbali wa afya na viongozi wa kijamii juu ya upimaji na utambuzi wa dalili za kansa ya shingo ya kizazi na utoaji wa huduma bora za afya kwa mama na mtoto.

Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt. Rena kapinga alisema kuwa hospitali hiyo itatoa huduma ya upasuaji wa watoto waliozaliwa na ulemavu pamoja na huduma za majeruhi.

“Jengo hili ambalo tumekabidhiwa likiwa na vifaa tiba lina uwezo wa kufanya zoezi la upasuaji kwa wagonjwa wawili kwa wakati mmoja pomoja na miundombinu na mifumo yake ambapo matarajio yetu makubwa ni kupata usajili wa kuwa hospitali ya wilaya kwani miundombinu imekamilika,”alisema Dkt. Kapinga.

Alisema kuwa kupitia barua yao yenye kumb. Na. H.213/290,02 ya Oktoba 25, 2010 Halmashauri hiyo inatarajia kuwa wizara mama ya Afya na Ustawi wa jamii itaanza kukipatia kituo hicho dawa na vifaa tiba kwa ngazi ya Hospitali kama ilivyoridhiua ili kujenga uwezo wa kuhudumia wagonjwa wengi ambao wapokatika makundi ya msamaha kwa mujibu wa sera.

Askofu Mkuu wa Jimbo la Musoma Hilkiah Omindo alisema kuwa kanisa lipo katika jamii hivyo shida ya jamii ni shida ya kanisa hivo upendo wa mungu umeisukuma kanisa hilo kujitolea na kuweza kujenga jingo hilo na kutoa vifaa tiba.

“Tunaomba serikali na kanisa kushirikiana bega kwa bega katika kuhudumia jamii katika masuala mbalimbali hasa kwenye afya zao pia tunaishukuru serikali kutupatia msamaha wa vifaa hivyo ambapo kama tungelipa ushuru tungeshindwa kuvitoa bandarini,”alisema Askofu Omindo.

 Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira alisema kuwa maendeleo ni mchakato hivyo hayaji kama mvua zinavyonyesha pia kuwaomba watumishi wa hospitali hiyo kutoa huduma kwa jamii kwa upendo na kutumia lugha mzuri kwa wagonjwa.

“Wahudumieni vizuri wagonjwa wanaokuja hapa kwa kutumia lugha mzuri serikali inajua mna matatizo mengi yanayowakabili ila inajitahidi kuwa karibu nanyi ili kujaribu kupunguza matatizo yenu ya kiuchumi,”alisema Wassira.

Hospitali ya Manyamanyama ilikuwa ni kituo cha Afya na kilianzishwa miaka ya 70 na awamu ya kwanza ya mradi huo ulianza Desemba 2010 hadi novemba 2011 na awamu ya pili ya mradi ya kupanua kituo hicho na kuwa Hospitali ya  wilaya ilianza Mei 2012  na kumalizika Aprili 31 mwaka huu.  

MWISHO

                                                                       

0 comments:

Post a Comment