Monday, October 21, 2013

UCHOMAJI MOTO MISITU WILAYA YA NANYUMBU SASA WAVALIWA NJUGA TAASISI ZAANZA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI WA WILAYA HIYO



Na Thomas Dominick,

Nanyumbu



BAADA ya Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Festo Kiswaga kutangaza kuwa uchomaji moto misitu ni janga la wilaya hiyo taasisi mbalimbali zimeanza kutoa mafunzo juu ya athari za uchomaji moto misitu kwa kushirikiana na Halmashauri hiyo.



Akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake jana, Afisa Misitu wa wilaya hiyo Fokas Mlelwa alisema kuwa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu ambayo makao makuu yake yapo Wilayani Masasi wameweza kutoa elimu katika vijiji vinne vinavyozunguka Misitu ya Taifa za Ndechela na Mbangara.



Alisema kuwa vijiji vilivyonufaika na mafunzo hayo ni kijiji cha Mburusa na Chimika vilivyo katika hifadhi ya Ndechela na kijiji cha Marumba na Mbangara Mbuyuni vilivyo katika hifadhi ya Mbangara.



“Mafunzo yetu yameshirikisha rika mbili za wazee na vijana ambapo kila kijiji kilifanya mafunzo kwa siku moja ambapo tulianza na wazee 10 kisha vijana 10 ambapo mada kuu ilikuwa moto na jamii,”alisema Mlelwa.



Alisema kuwa kundi la wazee walifundishwa na kulenga kupunguza matukio ya moto na wazee hao waliweka mikakati mbalimbali pamoja na kuunda kamati za kusimamia na kupunguza matukio ya moto katika maeneo yao.



Pia alisema kuwa vijana nao walifundishwa masomo kama ya wazee lakini ya ziada walifundishwa mbinu mbalimbali za kukabiliana na moto unapotokea na kuuzima, pia mbinu ya namna ya kuuzima moto, vifaa, namna ya kumuokoa mtu aliyezingirwa na moto na mbinu ya kujiokoa mwenyewe na moto.



Alisema kuwa uchomaji wa moto misitu unasababisha harasa kubwa kwa jamii ambapo huatarisha uhai wa watu, mali na mzaingira yao, vyanzo vya maji hubakia wazi na kusababisha kukauka, uoto wa asili unapotea na uhai wa viumbe hai nao unapotea.



Alipoulizwa kuwa mafunzo hayo yatasaidia kumaliza tatizo la uchomaji moto misitu mwakani na kunahatua gani watavifikia vijiji vingine Mlelwa alisema kuwa mafunzo hayo hayataweza kutokomeza kabisa tatizo la uchomaji moto lakini yatasaidia kupunguza matukio ya moto ambayo yameshamiri wilayani humo.



“Mpango wetu ni kuvifikia vijiji vyote vilivyopo wilaya yetu kwani tatizo hili linavikabili vijiji vingi sana katika wilaya yetu lakini tatizo la kifedha ndio kikwazo kikubwa kwetu lakini tukipata fedha tutafaya mafunzo hatua kwa hatua ili tuvifikie vijiji vyote na kutokomeza kabisa janga hili,”alisema Mlekwa.



     














0 comments:

Post a Comment