WILAYA NANYUMBU YAKATAA KUNG'OKA MKOANI MTWARA
*WAJUMBE WADAI MASLAHI BINAFSI KUZOROTESHA MAISSHA YA WANANCHI WAO ENDAPO WATAKUBALI KUHAMIA MKOA WA KUSINI.
* DC APIGILIA MSUMARI WA MWISHO
Na Thomas Dominick,
Nanyumbu.
WAJUMBE wa Kamati ya Ushauri
ya Wilaya (DCC) ya Wilaya ya Nanyumbu Mkoa wa Mtwara wamekataa ajenda ya kutaka
wilaya hiyo ikubali kujitenga kutoka katika mkoa wa Mtwara na kujiunga katika Mkoa
wa Kusini.
Ambapo wajumbe hao walitoa angalizo
kuwa endepo wilaya za Masasi, Liwale na Nanchingwea ambazo zinataka kuunda mkoa
wa kusini zikishinda basi wilaya ya Nanyumbu itaombe kujiunga katika Mkoa
mwengine Mpya wa Tunduru.
Wakizungumza katika kikao
hicho, wajumbe hao kwa pamoja walikubaliana kuwa hawana mpango wa kuhama katika
mkoa ingawa baadhi ya wilaya zinaishinikiza wilaya hiyo ikubaliane na matakwa
yao.
Katika mjadala huo Mwenyekiti
wa Halmashauri hiyo, William Dua alisema kuwa inashangaza kuona miaka mingi
iliyopita kabla ya kupatikana kwa gesi mchakato wa kuugawa Mkoa wa Mtwara ulifanyika
ila viongozi waliokuwepo walikataa kwa madai kuwa mkoa huo ni mdogo.
“Kinachoshangaza mchakato huu
sasa umekuwa wa kulazimishana tukubali kuondoka baada ya kuona kuwa kuna gesi
imepatikana maana ukienda kwenye vikao unaambiwa nendeni mkajadiliane mapema
ili tuwapeni kibali kuna nini hapa? Alihiji Dua.
Dua aliwataka wajumbe
wafikirie kwa umakini zaidi bila kuwaumiza wananchi wao kwani kujitenga na
kuunda mkoa mpya wa Kusini ni dhahiri kuwatakia wananchi wao maisha ya
umasikini uliokidhiri wakati neema imefunguka ndani ya mkoa huo.
Pia Joseph Omary alisema kuwa
kujitoa katika mkoa wa Mtwara ni kukimbia Baraka na kukimbilia balaa kwani kwa
sasa dunia inaiangalia Mtwara kutokana na utajiri wa gesi iliyopo.
“Huu sio muda muafaka kwa
wilaya changa ya Nanyumbu kukubaliana na matakwa ya wachache kujiondoka katika Baraka
ambayo mungu ameishusha katika Mkoa wetu tutazame maendeleo na sio siasa,”
alisema Omary.
Naye Diwani wa Kata ya
Mangaka Amina Likungwa alisema kuwa Kwenda katika Mkoa wa kusini ni kujipalia
makaa ya moto kwani katika mkoa huo mpya hakuna rasilimali ya kuwakomboa
wananchi wao.
Akikamilisha mjadala huo
ambao ulikuwa na vuta nikuvute Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga alisema kuwa
kama wilaya za Masasi, Liwale na nachingwea zitakuwa na nguvu wilaya ya
Nanyumbu itaomba kujiunga katika mkoa unaotarajiwa kuanzisha wa Tunduru kwani
huko kidogo kuna neema kwa wananchi wake.
“Endapo Wilaya hizi tatu zitakuwa
na nguvu tusiwakatalie lakini sisi kwa umoja wetu huu tuombe kujiunga katika
mkoa wa Tunduru ambako kuna fursa mbalimbali za kimaendeleo kwa wananchi wetu
na sio Mkoa wakusini ambao ni ina ardhi kame,”alisema Festo.
Alisema kuwa Mkoa wa Mtwara utakuwa
kwa kasi kubwa baada ya wawekezaji wengi kuja kuwekeza mkoani humo ambapo
alitaja kuwa kuna kiwanda cha sementi kikubwa Afrika kimeshajengwa
kinachomilikiwa na Dangote tajiri mkubwa Afrika, Kiwanda cha mbolea na kiwanda
cha dawa ambacho nacho kipo njiani kujengwa kwa kushirikiana na serikali ya
Ujerumani hivyo kujiondoa kutoka Mtwara ni kukimbilia umasikini.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment