Saturday, February 2, 2013

UNYAMA WAENDELEA MUSOMA MWINGINE ANYONGWA CHUPI YAOKOTWA PEMBENI YA MWILI WA MAREHEMU




 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Absalom Mwakyoma
 
Na Thomas Dominick,
Musoma

MTU mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja mkazi wa Buhare Mgaranjabo, Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara alikutwa amekufa kwa kunyongwa na kanga shingoni na mwili wake kutupwa kichakani na watu wasiojulikana.

Taarifa liyotolewa kwa vyombo vya habari nchini na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Absalom Mwakyoma zilisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 31 mwaka huu saa 4:15 jioni.

Taarifa zinasema kuwa kando ya mwili wa marehemu ilikutwa chupi, skin tight zimechanwa, dumu la kuchotea maji likiwa mita 20 tokea mwili ulipokuwa.

Inadaiwa kuwa nywele za marehemu zilikutwa zikiwa zimefungwa kwenye kijiti kichakani hapo na kanga ikiwa shingoni huku ulimi wake ukiwa nje na kinyesi pembeni.

Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuwabaini waliofanya tukio hilo ili sheria ichukue mkondo wake.

Mwakyoma ametoa wito kwa wananchi watakaokuwa na taarifa za watu au mtu waliohusika na mauaji hayo watoe kwa siri kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili wauaji hao wachukuliwe hatua za kisheria.

Matukio ya mauaji yamekuwa kero kwa wananchi wa Mkoa wa Mara ambapo Wilaya ya Butiama imeongoza kwa mauaji ya kikatili ambapo jumla ya watu wanne waliuawa katika kipindi cha Novemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment