Madiwani wa Manispaa ya Musoma wakisikiliza Bajeti ya Fedha ya mwaka 2013/14 ambayo ilisomwa na mchumi wa Manispaa hiyo John Masero kisha kuipitisha.
Diwani wa Kamnyonge Angela Derrick akitoa hoja juu ya ujenzi wa Barabara ya Biafra iliyopo kwenye Kata yake iliyotengewa kiasi cha Milioni 7 hivyo kuomba iongezwe ili kazi ifanyike kwa ufanisi mkubwa na kumaliza tatizo la barabara hiyo.
Na Thomas Dominick,
Musoma
MANISPAA ya Musoma imepitisha bajeti ya fedha ya mwaka
2013/14 Manispaa hiyo inatarajia kupata jumla ya shilingi Bilioni 19.751 ambayo
imewekwa katika vipaumbele muhimu vitano.
Akisoma bajeti hiyo juzi Mchumi wa Manispaa hiyo, John
Masero alisema kuwa vipaumbele hivyo ni pamoja na kuboresha elimu ya msingi na
sekondari kwa kuhakikisha tatizo la upungufu wa madawati linatatuliwa na
kuendelea kujenga matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na
maabara.
“Pamoja na hayo juu vipaumbele vingine ni pamoja na Kuongeza
ufanisi katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na vyanzo vyetu wenyewe,
kuboresha huduma za kiuchumi kwa kukarabati barabara za manispaa na masoko,
kuporesha huduma za afya kwa kuongeza ufanisi na upanuzi wa huduma,”alisema
Masero.
Vipaumbele kingine ni kuimarisha uhusiano na wadau
mbalimbali wa maendeleo pamoja na kutafuta wadau wengine wa ndani na nje ya
nchi wenye nia ya kuendeleza manispaa hiyo ya Musoma.
“Mheshimiwa Mwenyekiti katika kipindi cha fedha 2013/14
Manispaa yetu inatarajia kupata jumla ya shilingi Bilioni 19.751 ilinganishwa
na Bilioni 29.101 zilizokisiwi kwa kipindi cha mwaka 2012/13 ikiwa ni upungufu
wa Bilioni 9.350 upungufu huu umetokana na upungufu wa fedha za miradi ya
maendeleo,”alisema.
Masero alifafanua kuwa fedha hizo zitapatikana katika mapato
ya Halmashauri ambayo yatakuwa ni Bilioni 1.615 na Bilioni 18.135 kutoka
serikali kuu na wadau wengine. Ambapo Halmashauri hiyo itapata mapato kutoka vyanzo vya kodi
mbalimbali, ushuru wa huduma, leseni mbalimbali, leseni za pombe, karo za
wanafunzi shule za sekondari na mapato mengine.
Kwa upande wa matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2013/14
Manispaa hiyo imekisia kutumia Bilioni 12.111 kwa mishahara ambapo halmashauri
hiyo ina watumishi 1,477 walioko katika idara za utawala, fedha, elimu ya
msingi, elimu ya sekondari, mipango na uchumi, afya, ujenzi, mipango miji,
maendeleo ya jamii, kilimo na mifugo pia mwaka 2013/14 inatarajia kuajiri
watumisha wapya 207.
Baada ya kumaliza kusoma bajeti hiyo madiwani wa Manispaa
hiyo waliijadili kasha kuipitisha kwa pamoja na Diwani wa kamnyonge Angela
Derrick alilalamikia kutengewa fedha kidogo kwa ajili ya ukarabati wa barabara
ya Biafra yenye urefu wa kilomita 1 ambayo imetengewa shilingi milioni 7 ukilinganisha na kata zingine zenye
barabara za kilomita 2 zimetengewa shilingi milioni 20.
“Mheshimiwa mwenyekiti inasikitisha kuona kuwa Kata yangu
imetengewa shilingi milioni 7 kwa barabara yenye urefu wa kilomita 1 wakati
Kata zingine zenye barabara zenye urefu wa kilomita 2 wamepewa shilingi milioni
20 hapa hakuna usawa tugawane wote sawa hata kama kasungura kikiwa
kadogo,”alisema Angela.
Ambapo mchumi huyo alisema kuwa fedha za ujenzi wa barabara
zinaombwa kila mwaka mwaka hivyo zitajadiliwa tena mwaka wa fedha ujao ili
kumaliza tatizo la mtaa wa Biafra na sio kugombania fito wakati wanajenga
nyumba moja.
Mwisho Meya wa Manispaa hiyo Alex Kisurura aliwaomba
madiwani kuwaelimisha umuhimu wa kulipa kodi na fedha zitakazopelekwa kwenye
kata zao zifanye kazi za maendeleo ili wananchi waone faida ya kodi zao.
“Usimamizi wa fedha wa fedha za miradi uwe mzuri na
kuwashirikisha wananchi kwenye maamuzi pia wananchi nao walinde miradi hiyo”,
alisema Kisurura.
Kabla ya bajeti hiyo kupitishwa madiwani wa Manispaa hiyo
walilazimika kuitisha kikao cha dharura kilichofanyika Februari 16 mwaka huu kujua
nani alipitisha bajeti hiyo ambayo ilipelekwa waizarani Januari 31 mwaka huu bila
kupitia kwenye kamati mbalimbali za Manispaa kasha baraza la madiwani.
Hali hiyo iliyopelekea Meya kukalia kuti kavu hadi
Mkurugenzi Ahmed Sawa alipotoa ufafanuzi wa kutosha ambapo aliwaambia hali hiyo
ilitokana na mabadiliko ya Bunge la bajeti litakalofanyika mwezi Aprili mwaka
huu.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment