Wednesday, February 13, 2013

WATU SITA WAFA MKOANI MARA KWA MATUKIO MBALIMBALI

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) akitoa taari za matukio yaliyotokea Mkoani humo baada ya watu sita kufariki dunia kwa matukio mbalimbali.



Na Thomas Dominick,
Mara

Watu sita wamekufa katika matukio mbalimbali Mkoani Mara na wengine tisa wakijeruhiwa ambapo Wanawake watatu wamekufa baada ya kupigwa na waume zao.

Katika matukio hayo ni mauaji wanawake watatu waliouawa baada ya kupiga na waume zao akiwemo mmoja aliyepigwa kutokana na ugomvi wa Ndala (Kandambili).

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Japhet Lusingu alisema kuwa matukio hayo yametokea kati ya mwezi Januari na Februari mwaka huu.

Tukio la kwanza lilitokea Februari 10 mwaka huu saa 3:00 asubuhi katika kijiji cha Tonyo kata ya Busumwa, Wilaya ya Butiama , Mkoani humo baada ya mwanamke aliyetambulika kwa jina la Happyness Lucas (25), aliyepigwa na mume wake aliyejulikana kwa jina la Rugera John (27).

Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa ndala ( Kandambili) ambazo mume wa marehemu alikuwa amamnunulia mke mdogo, marehemu alipelekwa katika Hospitali ya Butiama kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini Februari 11 alifariki dunia.

Tukio jingine lilitokea Januari 28 Mwaka huu Wilayani Bunda, katika Mtaa wa Chiringe, Mtu mmoja Rhobi Lucas (24) fundi cherehani akiwa nyumbani kwake alifika mume wake aitwaye Masumbuko Khamis akiwa ameongozana na hawara yake Joyce Manumbu.

Inadaiwa kuwa baada ya kufika mume wake alianzisha ugomvi na kuanza kumshambulia mke wake kwa mateke huku akishirikiana na hawara yake. Baada ya ugomvi mwanamke huyo aliamua kuondoka nyumbani kwake na
kwenda nyumbani kwa wazazi wake siku hiyo hiyo na alikwenda kutoa taarifa ya kushambuliwa.

Kamanda Lusingu alisema kuwa Januari 30 mwaka huu  naye Masumbuko alifika Polisi na kutoa taarifa kuwa ameshambuliwa na mke wake na baada ya taarifa hiyo mke wake alikamatwa na Januari 31 alifikishwa mahakamani.

Alisema kuwa februari 9 mwaka huu mwanamke huyo alizidiwa na hali yake kuwa mbaya kutokana na kipigo alichopigwa na mume wake kwa kushirikiana na hawara yake na kupelekwa Hospitali ya DDH Bunda kwa
matibabu lakini Februari 11 alifariki dunia. Jeshi hilo linamshikilia mwanaume huyo kuhusiana na kifo hicho.

Tukio la tatu, lilitokea Februari 11, mwaka huu saa 1:30 asubuhi maeneo ya Kijiji cha Mkirira wilaya ya Butiama, mwanamke aliyejulikana kwa jina la Ziada Sasita (35) mkazi wa kijiji cha Kabegi aliuawa kwa kunyongwa shingo yake kwa kutumia nguo yake mtandio hadi kufa na watu wasiojulikana.

Marehemu alikuwa anatokea kwa mjomba yake maeneo ya mkirira ambako alikuwa ameenda kumsalimia na siku ya tukio alikuwa anarudi kabegi ambako alikuwa ameolewa. Mwili wa marehemu ulikutwa na mtandio shingoni na ulimi wake ukiwa umetoka nje.

Hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.

Tukio la nne lilitokea Februari 9 mwaka huu saa 9:00 jioni katika kijiji cha Nambubi Tarafa ya Nansimo wilayani Bunda Mkoani humo mwanamke aliyejulikana kwa jina la Edith Christopher (36) alishambuliwa kwa kupigwa na mpini wa mundu tumboni, mgongoni na kifuani na kufariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali.

Mtuhumiwa wa tukio hilo ni mume wa marehemu aitwaye Elephasi Maitabo (58) mtuhumiwa amekamatwa na polisi na atafikishwa mahakamani mara taratibu zitakapokamilika na chanzo cha mauaji hakijajulikana.

Tukio la tano,  ni la ajali ya mwendesha pikipiki kugonga kizuizi cha standi mpya ya mabasi wilayani Bunda ambapo mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Maka mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 20 akiwa na pikipiki ambayo haikuwa na namba ya usajili, chanzo cha tukio hilo ni mwendo kasi wa mwendesha pikipiki.

Tukio la mwisho ni lilitokea Februari 10 mwaka huu saa 4:15 usiku katika kijiji cha Msinganyi wilayani Bunda  ambapo gari aina ya Fuso lenye namba ya usajili T 677 BLQ mali ya Masunga Bugubugu mkazi wa Bariadi iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina lake hadi sasa.

Gari hiyo ilikuwa inatokea kijiji cha Kenyamonta wilaya ya Serengeti ambako kulikuwa na mnada iliacha njia njia na kupinduka na kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Magoti mwenye umri kati ya miaka 35 hadi 40 mdfanyabiashara mkazi wa makutano wilaya ya Butiama na wengine tisa kujeruhiwa.

Kamanda Lusingu aliwataja waliojeruhiwa ni Grace Masoka (40), Prisca Gwasi (42), Chausiku Mashara (35), Neema Hamis (25), Chacha Mwita (34), jamwela Wambura (30), Hassan Bunge (34), Juma Komba (22) na mary Rashid (37) wote wakazi wa Wilayani Bunda.

Kamanda Lusingu ametoa wito kwa wanaume wa Mkoa wa Mara kuacha kutumia nguvu na mabavu kwa wake zao kwani matukio ya aina hiyo yamezidi, pamoja na madereva wanaoendesha magari na pikipiki kuwa waangalifu
wanapoendesha vyombo hivyo ilikuepusha ajali zinazosababisha vifo na majeruhi.

MWISHO

 

0 comments:

Post a Comment