Friday, February 22, 2013

CHADEMA MUSOMA YACHAFUKA MADIWANI WAFUKUZWA





  Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya  Meshack Rutantongani akisoma na kuelezea vifungu vya katiba ya CHADEMA baada ya kuamua kuwatimua madiwani wake wawili wa viti maalumu na Meya na wenzake wawili kupewa siku 14 kujieleza.

 Ofisi za chadema Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara

* Waliofukuzwa wasema hawatishiki 
* Wasema kilichofichwa kitafichuka 
* wadai zama za Chama zimefika mwisho
*Maslahi binafsi ndio chanzo cha mgogoro ndani ya chama hicho 

Na Thomas Dominick,
Musoma

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara kimewavua uanachama madiwani wawili wa viti maalumu na madiwani wengine watatu akiwemo Meya wa Manispaa Alex Kisurura kuandikiwa hati ya mashitaka na kutakiwa kujieleza  ndani ya siku 14 na baada ya hapo kikao kingine kitaitishwa kupitia maelezo yao ili hatua stahiki zichukuliwe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mwenezi wa Wilaya hiyo Meshack Rutantongani alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kwenye kikao cha kamati tendaji ya Wilaya kilichokaa Februari 21 mwaka huu na kufikia maamuzi hayo kutokana na utovu wa nidhamu wa madiwani hao.

“Chadema ni taasisi inayoendeshwa kwa katiba na kanuni zake ukisoma utakuta kuna mambo ambayo mwanachama au kiongozi hatakiwi kuyafanya kwa hivyo hawa wameenda kinyume na chama hivyo tumeamua wawili kuwafuta uanachama na hwo wengine wajieleze,”alisema Rutantongani.

Aliwataja madiwani wa viti maalumu waliovuliwa uanachama ni Habiba Ally na Miriam Daudi na waliondikiwa barua za kujieleza ni pamoja na meya Alex Kisurura ambaye pia ni diwani wa kata ya Nyamatare, Haile Siza Tarai diwani wa Kata ya kitaji na Angela Derrick diwani wa kata ya kamnyonge.

Alisema kuwa madiwani hao waliitwa kwenye kikao hicho lakini waligoma kuhudhuria ambapo hiyo nayo ni sehemu ya utovu wa nidhamu kwa kukataa wito wa kamati hiyo ambayo ni chombo kikubwa ndani ya chama hicho.

“Tumezingatia Kanuni za katiba ibara ya 5.66, 6.34 na 6.36 na tumefuata Ibara ya 11 kifungu cha I, II, III, IV, V, VI, VII, VIII, IX, X vyote hivyo vinazungumzia jinsi gani wanachama au kiongozi akifanya kosa hatua za kumchukulia,”alisema.

Alisema kuwa madiwani hao wamekuwa wakifanya makosa kwa kipindi kirefu na wamewahi kuitwa kwa ajili ya kujieleza pamoja na kupewa onyo lakini wamekuwa wakaidi na kurudia kufanya makosa.

Pia viongozi hao wamekuwa wakimpigia simu Katibu Mkuu Dr. Wilbroad kumuelezea mambo ya uongo kwa ajili ya kuwachonganisha naye kitendo ambacho wanadai kuwa kimewaudhi pia alisema kuwa pale wanapopigia simu Dr. Slaa anarudisha kwa viongozi hao.

Gazeti hili lilifanya mahojiano na baadhi ya madiwani hao ambapo Diwani wa kamnyonge angela Derrick alisema kuwa sababu ya kuandikiwa barua ya kujieleza kutokana na kutounga mkono mbinu yao ya kumuondoa Meya wa manispaa hiyo.

“Tunakubaliana, kwani wao sio waliotuleta hapa tumechaguliwa na kundi kubwa la wananchi na sio wao ambao wanataka maslahi yao binafsi yafanikiwe na hatupo kwenye chama kwa ajili ya kuendesha migogoro lakini hukumu ya shetani ni aibu, mungu atawaonyesha mambo yaliyojificha ndani ya chama na maslahi ambayo watu wanapigania kwa ajili ya kujinufaisha,”

“Mungu siku moja ataonyesha hukumu ya shetani na ukweli utaonekana kwa ubaya wao wanayotaka kuyatekeleza wananchi wawe wavumilivu kwa taarifa hizi lakini ukweli utafunuliwa,” alisema Angela.

Pia Diwani aliyevuliwa uanachama Habiba Ally hajui chochote anachoyambua kuwa ni Diwani halali wa  kwa kuwa hajapata barua kutoka kwenye chama.

“Hizo ni Propaganda zao tu kwa maslahi yao na kikundi kidogo ambacho kinataka maslahi yao yaimarike kutoka kwenye jasho la wananchi wa Musoma hivyo tumekuwa hatutaki kuwaunga ndio maana wanasema hatuna nidhamu ebu waulizeni ni kosa gani tumefanya kama watawapa majibu,”alisema Habiba.

Meya Alex Kisurura alisema kuwa hana taarifa ya kikao hicho na hajui kilifanyika lini kwa lengo gani lakini alisema kuwa mambo yanayotokea ndani ya Chadema ni kutokana na maslahi ya watu wachache ambao wanataka kujinufaisha kupitia kwenye chama hicho.

Juhudi za kumpata Katibu Mkuu wa Chama hicho Dr. Wilbroad Slaa ili kuzungumzia mgogoro uliopo ndani ya chama hicho katika Manispaa ya Musoma ambapo simu yake iliita bila kupokelewa.

Viongozi wa Chadema Musoma wanadai kuwa viongozi hao waliosimamishwa wamekuwa wakimpigia simu kumueleza mambo ya uongo. 


MWISHO

0 comments:

Post a Comment