Monday, February 4, 2013

MUSOMA YAPATA MAFANIKIO KIUCHUMI






 Waandishi wa habari Bigambo Jeje akipata kinywaji wakati wakisubiri mkutano wa waandishi wa habari na Mkuu wa Wilaya Musoma Jackson Msome pembeni ni mwandishi mwingine Fazel Janja.
 Mwakilishi wa Sahara Media Mkoa wa Mara, Dick Mohamed akiwa anawajibika wakati wa mkutano wa waandishi wa habari na Mkuu wa Wilaya Musoma Jackson Msome.
 Mwandishi wa Mtanzania Shomari Binda na Pascal Buya wakiwa katika mkutano wa waandishi wa habari na Mkuu wa Wilaya Musoma Jackson Msome. Aliyekuwa akiwaeleza mwananchi wa Wilaya hiyo mafanikio ya serikali ya awamu ya Nne tangu Novemba mwaka 2005 hadi Desemba 2012.
 Mkuu wa Wilaya ya Musoma Jackson Msome akisoma mafanikio yaliyopatikana katika Wilaya hiyo chini ya Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Na Thomas Dominick,
Musoma

MANISPAA ya Musoma Mkoa wa Mara imeongeza mapato ya ndani hadi kufikia Shilingi Bilioni 1.039 Desemba mwaka 2012 sawa na asilimia 184.98 ukilinganisha mapato yaliyopatikana Novemba mwaka 2005 yaliyokuwa sh. Milioni 364.836/=.

Akisoma taarifa ya mafanikio hayo Mkuu wa Wilaya hiyo, Jackson Msome mbele ya waandishi wa habari ofisni kwake alisema kuwa katika kipindi hicho Manispaaa hiyo imeongeza ruzuku toka serikali kuu hadi kufikia Bilioni 11.862 sawa na asilimia 316.94 ukulinganisha mwaka 2005 ambapo ruzuku ilikuwa sh. Billion 2.845.

Msome alisema kuwa kutokana na kipato hicho Manispaa hiyo ina lengo la kupunguza utitiri wa vyanzo vya mapato visivyo na tija ambavyo ni kero kwa wananchi na kuwa na vyanzo vichache vyenye tija.

“Manispaa yetu ina jumla ya vyanzo vya mapato 17 vya ndani na hii baada ya kupunguza vyanzo vya mapato visivyo na tija lakini tumeweza kupata mafanikio makubwa katika makusanyo yetu ya ndani,”alisema Msome.

Alisema kuwa kutokana na juhudi za Serikali pato la mkazi kwa mwaka limeongezeka katika kipindi hicho kutoka wastani wa shilingi 268,000/= mwaka 2005 hadi 602,000/= mwaka 2012 sawa na asilimia 225.

Alisema kuwa kupanda kwa pato hilo ni kutokana na wananchi wengi kujitokeza kufanya shughuli za ujasiriamali kwa kuchukua mikopo katika mashirika na taasisi za kifedha zilizopo ambapo idadi ya wanaofanya biashara rasmi wenye leseni wameongezeka kutoka 357 mwaka 2005 hadi 4659 mwaka 2012 sawa na asilimia 120.5.

Kwa upande wa afya zahanati zimeongezeka toka 15 mwaka 2005 hadi 22 mwaka 2012 kutokana na ufanisi wa utoaji wa huduma hiyo asilimia ya utoaji chanjo kimepanda toka 85 hadi 98 Desemba 2012.

“Aidha katika kuthibiti malaria serikali iligawa vyandarua kwa kaya zote kwa asilimia 100 pia madaktari na wauguzi wameongezeka toka 12 hadi 25 mwaka 2012, pamoja na mpango wa kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya rufaa ya Kwangwa umekamilika na shughuli zitaanza hivi karibuni,”alisema Msome.

mwisho

0 comments:

Post a Comment