Na Thomas Dominick,
Nanyumbu
BAADA ya Mkuu wa Wilaya ya
Nanyumbu Festo Kiswaga kutangaza kuwa uchomaji moto misitu ni janga la wilaya
hiyo taasisi mbalimbali zimeanza kutoa mafunzo juu ya athari za uchomaji moto
misitu kwa kushirikiana na Halmashauri hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa
habari ofisini kwake jana, Afisa Misitu wa wilaya hiyo Fokas Mlelwa alisema
kuwa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu ambayo
makao makuu yake yapo Wilayani Masasi wameweza kutoa elimu katika vijiji vinne vinavyozunguka
Misitu ya Taifa za Ndechela na Mbangara.
Alisema kuwa vijiji
vilivyonufaika na mafunzo hayo ni kijiji cha Mburusa na Chimika vilivyo katika
hifadhi ya Ndechela na kijiji cha Marumba na Mbangara Mbuyuni vilivyo katika
hifadhi ya Mbangara.
“Mafunzo yetu yameshirikisha
rika mbili za wazee na vijana ambapo kila kijiji kilifanya mafunzo kwa siku
moja ambapo tulianza na wazee 10 kisha vijana 10 ambapo mada kuu ilikuwa moto
na jamii,”alisema Mlelwa.
Alisema kuwa kundi la wazee
walifundishwa na kulenga kupunguza matukio ya moto na wazee hao waliweka
mikakati mbalimbali pamoja na kuunda kamati za kusimamia na kupunguza matukio
ya moto katika maeneo yao.
Pia alisema kuwa vijana nao
walifundishwa masomo kama ya wazee lakini ya
ziada walifundishwa mbinu mbalimbali za kukabiliana na moto unapotokea na
kuuzima, pia mbinu ya namna ya kuuzima moto, vifaa, namna ya kumuokoa mtu
aliyezingirwa na moto na mbinu ya kujiokoa mwenyewe na moto.
Alisema kuwa uchomaji wa moto
misitu unasababisha harasa kubwa kwa jamii ambapo huatarisha uhai wa watu, mali
na mzaingira yao, vyanzo vya maji hubakia wazi na kusababisha kukauka, uoto wa
asili unapotea na uhai wa viumbe hai nao unapotea.
Alipoulizwa kuwa mafunzo hayo
yatasaidia kumaliza tatizo la uchomaji moto misitu mwakani na kunahatua gani
watavifikia vijiji vingine Mlelwa alisema kuwa mafunzo hayo hayataweza
kutokomeza kabisa tatizo la uchomaji moto lakini yatasaidia kupunguza matukio
ya moto ambayo yameshamiri wilayani humo.
“Mpango wetu ni kuvifikia
vijiji vyote vilivyopo wilaya yetu kwani tatizo hili linavikabili vijiji vingi sana katika wilaya yetu
lakini tatizo la kifedha ndio kikwazo kikubwa kwetu lakini tukipata fedha
tutafaya mafunzo hatua kwa hatua ili tuvifikie vijiji vyote na kutokomeza
kabisa janga hili,”alisema Mlekwa.