Monday, October 21, 2013

NDONDOCHA HAI APATIKANA KIJIJI CHA LUKULEDI WILAYA YA MASASI MKOA WA MTWARA TAFARANI KUBWA YAZUKA POLISI WAKANA KUHUSIANA NA TUKIO HILO



Na Thomas Dominick,
Masasi

Hali ya wasiwasi imeikumba kijiji cha Lukuledi Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara baada ya kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Said Nitole (18) ambaye alipotea katika mazingira ya utatanishi takribani miaka mitatu na kudaiwa kuchukuliwa ndondocha amepatikana akiwa amefungwa dawa kifuani, kiunoni na sehemu za siri.

Wakingumza na mwandishi wa habari kijijini hapo mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni mwanamgambo aliyejitaja kwa jina la Bonifance Lukas na mwalimu wa Shule ya msingi Lukuledi Rita Mbunda walisema kuwa tukio hilo lilitokea Octoba 18 mwaka huu baada ya kijana huyo kufika kwa mganga wa kienyeji aliyejulikana kwa jina la Mama Kongo na kulia kama paka kisha kutoweka.

Walidai kuwa siku ya pili octoba 19 saa moja usiku alifika tena kisha kuongea kwa lugha ya ishara ambapo mganga huyo alifanya dawa zake na kumdhibiti asitoweke kisha alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa serikali ya kijiji Said Makota na kituo kidogo cha polisi.

“Baada ya kutoa taarifa watu wengi walikusanyika na mimi kama mwanamgambo wa kijiji nilimchukua sambamba na viongozi pamoja na askari polisi hadi kituoni kwa mahojianao zaidi,”alisema Lucas.

Alidai kuwa baada ya mahojiano kijana huyo alisema kuwa alikuwa kwa mmoja wa wafanyabiashara yeye na wenzake wengine wengi wakimfanyia kazi mbalimbali ikiwemo kazi za kilimo na kuokota korosho ambapo alisema kuwa kwa siku yeye peke yake alikuwa anaokota debe tano,

Wananchi waliofika eneo la kituoni walipandisha jazba na kuomba uongozi wa kijiji pamoja na askari wawapeleke walipo ndondocha wengine ili waweze kuwatoa kisha kumfanyia kitu kibaya mhusika wa matukio hayo.

Mkuu wa kituo hicho baada ya kuona hali ni tete aliomba msaada kutoka kituo kikuu cha Polisi wilayani Masasi kwa ajili ya kuweka ulinzi pamoja na kumchukua kijana huyo kwa mahojiano zaidi.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho Said Makota naye alikiri kuwa tukio hilo la kushangaza lilitokea kijiji hapo ambapo mzazi wa kijana huyo aliyemtaja kwa jina la Rashid Nitole aliwahi kutoa taarifa za kupotea kwa kijana wake katika mazingira ya utatanishi kisha kupatiwa kibali cha kumtafuta sehemu mbalimbali.

“Lakini baada ya kupatikana kwa kijana huyo mwishoni mwa wiki tulimtafuta mzazi wa mtoto huyo na baada ya kufika alimtambua mtoto wake na mtoto alimtambua baba yake kisha walikumbatiana,”alisema Makota.

Alisema kuwa madai ya kuwa alikuwa kwa mmoja wa wafanyabiashara wa kijiji hicho mwenyekiti huyo alipinga na kusema kuwa ndondocha huyo alitokea kwa mganga wa kienyeji na sio kwa mfanyabiashara.

Taarifa kutoka kituo kikuu cha Polisi Wilaya ya masasi zilisema kuwa wao walienda kutoa ulinzi lakini hawawezi kulisemea suala hilo kwani polisi halihusiani na masuala ya kishirikina.



































0 comments:

Post a Comment