Thursday, October 9, 2014

NANYUMBU YAKATAA KUNG'OKA MKOA WA MTWARA WAUKANA MKOA WA KUSINI



WILAYA NANYUMBU YAKATAA KUNG'OKA MKOANI MTWARA
 
 *WAJUMBE WADAI MASLAHI BINAFSI KUZOROTESHA MAISSHA YA WANANCHI WAO ENDAPO WATAKUBALI KUHAMIA MKOA WA KUSINI.
 * DC APIGILIA MSUMARI WA MWISHO


Na Thomas Dominick,
Nanyumbu.

WAJUMBE wa Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) ya Wilaya ya Nanyumbu Mkoa wa Mtwara wamekataa ajenda ya kutaka wilaya hiyo ikubali kujitenga kutoka katika mkoa wa Mtwara na kujiunga katika Mkoa wa Kusini.

Ambapo wajumbe hao walitoa angalizo kuwa endepo wilaya za Masasi, Liwale na Nanchingwea ambazo zinataka kuunda mkoa wa kusini zikishinda basi wilaya ya Nanyumbu itaombe kujiunga katika Mkoa mwengine Mpya wa Tunduru.

Wakizungumza katika kikao hicho, wajumbe hao kwa pamoja walikubaliana kuwa hawana mpango wa kuhama katika mkoa ingawa baadhi ya wilaya zinaishinikiza wilaya hiyo ikubaliane na matakwa yao.

Katika mjadala huo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, William Dua alisema kuwa inashangaza kuona miaka mingi iliyopita kabla ya kupatikana kwa gesi mchakato wa kuugawa Mkoa wa Mtwara ulifanyika ila viongozi waliokuwepo walikataa kwa madai kuwa mkoa huo ni mdogo.

“Kinachoshangaza mchakato huu sasa umekuwa wa kulazimishana tukubali kuondoka baada ya kuona kuwa kuna gesi imepatikana maana ukienda kwenye vikao unaambiwa nendeni mkajadiliane mapema ili tuwapeni kibali kuna nini hapa? Alihiji Dua.

Dua aliwataka wajumbe wafikirie kwa umakini zaidi bila kuwaumiza wananchi wao kwani kujitenga na kuunda mkoa mpya wa Kusini ni dhahiri kuwatakia wananchi wao maisha ya umasikini uliokidhiri wakati neema imefunguka ndani ya mkoa huo.

Pia Joseph Omary alisema kuwa kujitoa katika mkoa wa Mtwara ni kukimbia Baraka na kukimbilia balaa kwani kwa sasa dunia inaiangalia Mtwara kutokana na utajiri wa gesi iliyopo.

“Huu sio muda muafaka kwa wilaya changa ya Nanyumbu kukubaliana na matakwa ya wachache kujiondoka katika Baraka ambayo mungu ameishusha katika Mkoa wetu tutazame maendeleo na sio siasa,” alisema Omary.

Naye Diwani wa Kata ya Mangaka Amina Likungwa alisema kuwa Kwenda katika Mkoa wa kusini ni kujipalia makaa ya moto kwani katika mkoa huo mpya hakuna rasilimali ya kuwakomboa wananchi wao.

Akikamilisha mjadala huo ambao ulikuwa na vuta nikuvute Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga alisema kuwa kama wilaya za Masasi, Liwale na nachingwea zitakuwa na nguvu wilaya ya Nanyumbu itaomba kujiunga katika mkoa unaotarajiwa kuanzisha wa Tunduru kwani huko kidogo kuna neema kwa wananchi wake.

“Endapo Wilaya hizi tatu zitakuwa na nguvu tusiwakatalie lakini sisi kwa umoja wetu huu tuombe kujiunga katika mkoa wa Tunduru ambako kuna fursa mbalimbali za kimaendeleo kwa wananchi wetu na sio Mkoa wakusini ambao ni ina ardhi kame,”alisema Festo.

Alisema kuwa Mkoa wa Mtwara utakuwa kwa kasi kubwa baada ya wawekezaji wengi kuja kuwekeza mkoani humo ambapo alitaja kuwa kuna kiwanda cha sementi kikubwa Afrika kimeshajengwa kinachomilikiwa na Dangote tajiri mkubwa Afrika, Kiwanda cha mbolea na kiwanda cha dawa ambacho nacho kipo njiani kujengwa kwa kushirikiana na serikali ya Ujerumani hivyo kujiondoa kutoka Mtwara ni kukimbilia umasikini.


MWISHO



Read More...