Saturday, August 17, 2013

SERIKALI YATANGAZA NEEMA KWA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI WA BUHEMBA WILAYA YA BUTIAMA MKOA WA MARA






 Baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao cha kutangaziwa neema kwa wachimbaji wadogo wa madini wa Buhemba Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Angeline Mabula.
Mkuu wa Wilaya ya Butiama Angeline Mabula akizungumza na viongozi na waandishi wa Habari hawapo pichani juu ya serikali kutenga maeneo kwa wachimbaji wadogo wa madini wa Buhemba.

Na Thomas Dominick,
Butiama.

SERIKALI imeshatimiza ndoto za wachimbaji wadogo baada ya kutangaza kukamilisha kazi ya upimaji wa viwanja 35 venye ukubwa wa hekta 9.64 katika eneo la Rwabasi na Mirwa katika machimbo ya Buhema Mkoani Mara.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari wilayani humo, Mkuu wa wilaya Angeline Mabula alisema kuwa utengaji wa maeneo hayo ni baada ya hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo kwenye bunge la bajeti 2013/14 kuwa wachimbaji hao wanatengewa maeneo rasmi ya uchimbaji.

“Kutokana na ari kubwa ya watafutaji wakubwa wa madini kuchukua leseni katika wilaya ya Butiama kumekuweko na uhaba wa maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo, Hali hii ilizua malalamiko kutoka kwa wachimbaji hao ambao waliomba kutengewa maeneo rasmi ya uchimbaji katika eneo la Buhemba,”alisema Mabula.

Alisema kuwa kabla ya upimaji huo eneo hilo lilifanyiwa uchunguzi wa Kijiolojia, Kijiofizikia na Kijiokemia na wataalamu kutoka wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kubaini kuwa eneo hilo lina miamba yenye dhahabu,”alisema.

Alisema kuwa zoezi hilo la upimaji lilikuwa shirikishi likihusisha wachimbaji na viongozi wa kata ya Buhemba na Mirwa ambapo kukamilika kwa zoezi hilo alitoa wito kwa wananchi wa Kata za Buhemba na Mirwa kutumia fursa hiyo vizuri kutuma maombi ya leseni kwa afisa madini mkazi wa Musoma kupitia vikundi vyao ushirika.

Pia aliwaagiza maafisa madini kuhakikisha kuwa leseni zinatayarishwa mapema kwa wale wote watakaoomba na wahusika wanaonyeshwa maeneo ya leseni zao kwa wakati, Pia alitoa wito kwa wachimbaji wadogo kujiepusha kabisa vitendo vya uvamizi wa maeneo yanayomilikiwa na watu wengine au mwekezaji, hususani eneo la STAMICO na mwekezaji Manjaro Resources ya nchini Australia.

Mabula aliwaomba wananchi wawe wavumilivu na watii wa sheria bila shurti hasa pale wanapokuwa na malalamiko kwa utatuzi wa kero zao unazingatiwa kwa kufuata sheria za nchi, ambapo pia aliahidi kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini kuendelea kuwatafutia wananchi maeneo zaidi ya uchimbaji.

Naye Kaminishi Msaidizi Madini Kanda ya Ziwa Salim Said Salim alisema kuwa ofisi yake itahakikisha wachimbaji wadogo wanapata leseni za madini ndani ya wiki moja bila kuwa na usumbufu wowote.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment