Friday, December 28, 2012

JK AITAKA TAWIRI KUHAKIKISHA MBWAMWITU WALIOFUNGULIWA WANAKUWA SALAMA MUDA WOTE.







 Rais Kikwete akisalimiana na Mfugaji wa Mbwamwitu Joseph Kaboya ambaye aliwatunza kwa miezi miwili Mbwa hao walichukulia huko Loliondo kwa ajili ya kuja kuongeza Idadi ya wanyama hao ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Mradi wa kwanza ulikuwa 30 Augosti mwaka huu ambapo Mbwamwitu 11 walitolewa na Mradi wa Pili ulikuwa Desemba 23 mwaka huu ambapo mbwamwitu 15 pia walitolewa.
 Rais Jakaya Kikwete akizungumza na waandishi wa habari katika Hifadhi ya Serengeti baada ya kufugua mradi ya pili wa Ufugaji wa Mbwamwitu 15 ambao wamefunguliwa kwa ajili ya kuongeza idadi ya wanyama hao katika hifadhi hiyo na kufikia 26, Mbwamwitu walipotea katika hifadhi hiyo miaka 1990 kutokana na magonjwa.
 Rais Kikwete akikata utepe kuashiria kuwa Mbwa mwitu 15 walifugwa ndani ya fansi hii baada ya kufugwa kwa miezi miwili ikiwa ni mkakati wa kuongeza wanyama hao ambao walipoea katika miaka 1990.
 JK akiwa na wajukuu zake mkono wake wa kulia wakiangalia jinsi Mbwamwitu (hawapo pichani) wakitoka ndani ya banda lao ambamo walikuwa wamefuygwa takribani kwa miezi miwili.

 Rais Kikwete akienda eneo lililotengwa maalumu kwa ajili ya kukata utepe kuashiria mradi wa awamu ya pili wa Mbwamwitutayari umekamilika na wapo tayari kufunguliwa na kuanza kuishi bila ya kufuygwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Na Thomas Dominick,
Serengeti


RAIS Jakaya Kikwete ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori
(TAWIRI) kuhakikisha Mbwamwitu waliofunguliwa rasmi katika mbuga ya Serengeti wanakuwa salama muda wote ili wasitoweke tena.


Mbwa hao waliochukuliwa eneo la Loliondo wamefugwa katika Hifadhi ya Taifa (TANAPA) kwa miezi mitatu hili likiwa ni kundi la pili lenye mbwamwitu 15 ambapo kundi la kwanza lilitolewa Agosti 30 mwaka huu likiwa na mbwamwitu 11 waliachiwa ndani ya hifadhi hiyo miaka ya 1980 ndani ya hifadhi hiyo kulikuwepo na mbwamwitu 500.


Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki wakati wakiruhusu kundi la pili la mbwamwitu 15 ambao walikuwa wamefugwa katika eneo la Nyamuma ndani ya hifadhi hiyo kwa ajili ya juhudi za kuwarudisha wanyama hao ambao walitopotea miaka ya 1990.


“Sina shaka na mbwa hawa ila ninachowaomba ni kuwalinda na
kuwahakikishia usalama, ni miaka mingi sasa ndani ya hifadhi hii
hakuna mbwamwitu,”alisema Kikwete.


Rais Kikwete alisema kuwa kukosekana kwa wanyama hao ndani ya hifadhi hiyo kumesababisha kukosekana kwa kivutio kingine muhimu ambapo watalii wanahitaji kuwaona.


“Nawapongeza sana TAWIRI, Vodacom, TANAPA na mashirika yaliyofadhili mradi huu wa mbwa mwitu hii itasaidia kuongeza kivutio muhimu sana kwa watalii hata Ikulu nayo ilichangia milioni 30 kutokana na umuhimu wa mradi huu, hivyo natoa rai kwa mashirika mengine nchini kujitokeza kusaidia mradi huu ili kuweza kuongeza mbwa mwitu ndani ya hifadhi,”alisema.


Naye Mkurugenzi wa wa TAWIRI Dokta Simon Mduma alisema kuwa kutoweka kwa wanyama hao ni kutokana na magonjwa mbalimbali ya mbwa ambapo ililazimu kutoa chanjo kwa mbwa walioko karibu na hifadhi hiyo ili kuweza kumaliza magonjwa hayo na kuwarudisha mbwamwitu.


“Lengo letu ni kuleta familia sita ambazo zitapitia katika mradi huu
ili kuweza kuwaafya wasiweze kurudi kule walikotoka katika maeneo ya Loliondo na wazoee maisha ya hidfadhi ya TANAPA na waweze kuzaa na kuongezeka ili kiwe kivutio cha ndani ya hifadhi,”alisema Dokta Mduma.


Alisema kuwa kuna changamoto ambazo wanakabiliana nazo ikiwa ni pamoja mashirika mengi kutofadhili mradi huo ambapo kwa sasa kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom ndio pekee iliyotoa ufadhili wa zaidi ya milioni 450.


Kutokana na kuruhusiwa kwa mbwamwitu hao sasa imeongeza na kufanya idadi ya wanyama hao kufikia 26 ndani ya TANAPA ambapo Agosti 30 mwaka huu waliachiwa 11 na mwishoni mwa wiki wameachiwa mbwamwitu 15.


MWISHO
Read More...

Saturday, December 22, 2012

MAUAJI MENGINE YATOKEA BUTIAMA MKOANI MARA





Na Thomas Dominick,
Butiama

MATUKIO ya kutisha ya kuchinjwa watu na kuondoka na vichwa wanaendelea kushamiri Wilayani Butiama Mkoa wa Mara Baada ya Mwanamke mwingine aliyejulikana kwa jina Tabu Makanya (68) Mkazi wa Kijiji cha Kwikuba kuuawa na watu wanne ambapo sasa idadi imefikia watu wanne wakiwepo wanawake watatu.

Mauaji hayo yalitokea yalitokea Desemba 21, mwaka huu saa 5:30 usiku ambapo wauaji hao walifika nyumbani kwa marehemu na kumshambulia kwa kumpiga na fimbo na bapa za panga sehemu mbalimbali ili kumlegeza mwili wake na baadaye kumchinja na kuchukua kichwa chake ambapo waliweka kwenye mfuko wa salphet.

Kutokana na kufuatana kwa matukio hayo wananchi na waendesha Pikipki waliandamana na kufika kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Absalom Mwakyoma ambapo aliwatuliza kisha kutawanyika na kurudi Hospitali ya Mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo Absalom Mwakyoma alisema kuwa wauaji hao wanajulikana lakini majina yao yamehifadhiwa hadi watakapokamatwa.

"Baada ya kuondoka kwa wauaji hao nyumbani kwa marehemu ndipo vijana waliopo kwenye nyumba hiyo uwani pamoja na majirani walipiga yowe na kuanza kuwafukuza na baada ya kuona wanazidiwa walikitupa kichwa hicho na kutokomea gizani kwenye vichaka,"alisema Mwakyoma.

Kamanda Mwakyoma alisema kuwa juhudi za kufuatilia wahusika zimeanza kwa nguvu zote mara tu baada ya tukio hilo kutokea lakini hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa.

Matukio hayo ya watu kuchinjwa Wilayani Butiama yamefikia manne hadi sasa ambapo Desemba 2, Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Blandina Peru alichinjwa na kuchukuliwa damu yake tu, ambapo watuhumiwa watatu wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.

"Katika tukio hili tuliwakamata watuhumiwa watatu na wameshakiri kuhusika na tukio hilo na majina yao ni Sura Siriro, Jani Magesa na Mgasa Nyarukama na tukio la Sabina Mkireri wa kijiji cha Kabegi, Kata ya Nyakatende wilayani humo watu sita wamekamatwa na wanahojiwa kuhusiana na tukio hilo,"alisema.

Tukio jingine ni la mwendesha Pikipiki maarufu Bodaboda Thomas Majengo ambaye ni Mkazi wa Kiara Manispaa ya Musoma alichinjwa kisha kunyang'anywa pikipiki hiyo.

Kamanda Mwakyoma alisema kuwa tukio lililofanywa na waendeshwa Pikipiki waliofika katika ofisi yake kwa ajili ya kuomba kuonana naye walikuwa wameagizwa maalumu kutokana na kukanusha idadi ya watu waliotangazwa kuuawa ya watu 17.

"Ninasema kuwa mtu yeyote ambaye atahamasisha watu kuandamana na kuvamia ofisi na kufanya vurugu hatasalimika mkono wa sheria lazima utampitia,"alisema.

Alisema kuwa wananchi wanatakiwa kutii sheria bila shuruti na yeyote atakaye jitokeza kwa ajili ya vurugu jeshi hilo halitajali anafanya kazi katika taasisi gani na kudai kuwa jeshi hilo halitaki kusuguana na wanasiasa kwani kusema jambo lolote ni haki yao na wapo kwenye uwanja wao.

MWISHO
Read More...

Thursday, December 20, 2012

BODA BODA WA MANISPA YA MUSOMA ACHINJWA WILAYANI BUTIAMA








 Wananchi na waendesha Pikipiki wa Manispaa ya Musoma wakiwa wamefurika kumuona marehemu Thomas Majengo Mtaa wa Kiara ambaye amechinjwa shingo kwa nyuma na kukatwa mguu wake wa kulia na watu wanaodaiwa kuwa majambazi katika kijiji cha Kisamwene Kata ya Butuguri wilaya ya Butiama kisha kunyang'anywa pikipiki yake.
 Waendesha Pikipiki wakiwa nje ya Hospitali ya Mkoa wa Mara wakiwa wamepigwa butwaa baada ya mwenzao Thomas Majengo mkazi wa Mtaa wa Kiara ambaye amechinjwa shingo kwa nyuma na kukatwa mguu wake wa kulia katika kijiji cha Kisamwene Kata ya Butuguri wilaya ya Butiama kisha kunyang'anywa pikipiki yake.

 Mwaendesha Boda Boda wakitoka Hospitali ya Mkoa wa Mara na kuelekea nyumbani kwa marehemu Thomas Majengo Mtaa wa Kiara ambaye amechinjwa shingo kwa nyuma na kukatwa mguu wake wa kulia katika kijiji cha Kisamwene Kata ya Butuguri wilaya ya Butiama kisha kunyang'anywa pikipiki yake.


 Daktari akimfanyia vipimo Marehemu Thomas Majengo ambaye ni mwendesha Pikipiki maarufu Boda boda Mkazi wa Kiara Kigera Manispa ya Musoma Baada ya kuchinjwa shingo kwa nyuma na kukatwa mguu wake wa kulia kisha kunyang'anywa pikipiki yake.




Na Thomas Dominick,
Musoma

KIJANA aliyetambuliwa kwa jina la Thomas Majengo (23-28) Mkazi wa Kiara Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara amechinjwa shingo kwa nyuma na kukatwa mguu wake wa kulia na kunyang’anywa Pikipiki na watu wanaodaiwa kuwa majambazi.

Tukio hilo lilitokea Desemba 19 mwaka huu saa 2:30 usiku ambapo inadaiwa kuwa mwendesha Pikipiki huyo alikodiwa na watu ambao hawajajulikana ili awapeleke Katika Wilaya ya Butiama katika kijiji cha Kisamwene Kata ya Butuguri.

Jeshi la Polisi lilipata taarifa la tukio hilo na kwenda kuchukua mwili wa marehemu ambapo baada ya kufika Mjini Musoma waendesha pikipiki wote waliandamana na hadi kufika katika hospitali ya Mkoa huo hali iliyosababisha usumbufu na hofu kwa watumiaji wengine wa barabara.

Mwandishi wa habari alifika kwenye ofisi ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa,  Japhet Lusingu  ambaye alisema kuwa hawana tarifa na tukio hilo na kusema kuwa kam kuna sehemu nyingine ya kwenda kuchukua taarifa basi mwandishi huyo afuatilie.

“Sisi hatujui chochote kile kama kuna sehemu nyingine ya kwenda kuchukua taarifa basi nenda,”alisema Lusingu.

Ilibidi mwandishi huyo aende Ofisi ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Dokta Iragi Ngerageza ambapo alisema kuwa naye hajapata tukio kama hilo hivyo kuahidi kufuatilia kutokana na kuwa taarifa aliyopata ni matukio mengine.

Safari haikuishia hapo kwa mwandishi ndipo alipokwenda hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti ya Hospitali hiyo ambapo alikutana na muhudumu wa jingo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Masatu ambaye alikubali kutoa ushirikiano na kutaja jina la marehemu.

MWISHO

Read More...

Sunday, December 16, 2012

MKUTANO WA BULEMBO MUSOMA WACHAFUKA

 *Risasi za moto zarindima polisi wadumisha ulinzi maeneo ya mjini
*Wanne wakamatwa
*Askari Polisi Mmoja ajeruhiwa ashonwa nyuzi tano kichwani

 Gari ya Polisi Musoma ikiwa katika harakati za kutuliza vurugu katika mkutano wa Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi CCM Taifa Abdalah Bulembo uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Mukendo Manispaa ya Musoma.
Askari Polisi wakishuka kwenye gari kwa ajili ya kudhibiti hali ya Amani kwenye viwanja vya shule ya msingi Mukendo wakati wa mkutano wa Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi CCM Taifa Abdalah Bulembo.

Askari Polisi wakivinjari kwenye viwanja vya shule ya Msingi Mukendo Baada ya kudhibiti Vurugu
Kijana ambaye hakujulikana mara moja jina lake akidhibitiwa na askari Polisi baada ya Kumkamata.

Wananchi wa Manispaa ya Musoma wakiwa wamebaki vinywa wazi baada ya rabusha kati ya Polisi na Vijana Katika viwanja vya Shule ya Msingi Mukendo Manispaa ya Musoma.

Thomas Dominick,
Musoma

HALI ya amani ilitetereka katika Mkutano wa hadhari ulioitishwa na Jumuia ya Wazazi CCM ya wilaya ya Musoma na kuhutubiwa na Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Taifa  Al haji Abdalah Bulembo baada ya Jeshi la Polisi kulazimika kutumia risasi za moto kutawanya vijana wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema waliokuwa wanataka kuvamia mkutano huo.

Chanzo cha vurugu hizo ni baada ya askari Polisi kujaribu kumdhibiti kijana mmoja kukamatwa akijiandaa kwenda kufanya fujo kwenye mkutano huo katika vurugu hizo mmoja alijeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitali ya Mkoa na kushonwa kasha kuruhusiwa.

Mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Mukendo Bulembo alisema kuwa wananchi wa Musoma walikuwa na haki ya kuchagua Chadema katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ili waonje machungu ya upinzani.

Alisema kuwa tayari Serikali ipo tayari kuifungia Manispaa hiyo
kuipatia fedha za ruzuku toka Serikali kuu kwa kuwa fedha ambazo
zilitolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo fedha hizo ziliamishiwa
kwenye ujenzi wa Mitaro.

“Fedha ya Serikali kuu inapitishwa na Bunge hairuhusiwi kuguswa au kupelekwa kwenye mradi mwingine kufanya hivyo ni kosa, hapa Serikali kuu ilitoa fedha ya Ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa Barabara lakini fedha hizo zimetumika kwa mambo tofauti na Serikali
ilivyoagiza,”alisema Bulembo.

Bulembo alisema kuwa Serikali inaleta Mkaguzi Mkuu wa fedha za
Serikali ili kufanya ukaguzi wa kina kwa fedha za miradi ili kuona
uozo uliopo ndani ya Manispaa hiyo na kuwahakikishia wananchi baada ya muda mchache watasikia kesi zikiunguruma Mahakamani kutokana na Viongozi kutafuna fedha za Umma bila hofu.

Pia alijibu hoja liyotolewa na Viongozi wa Chadema za Mkuu wa wilaya kutohudhuria kikao chao kwa madai kuwa alikuwa katika m,ahadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania yaliyofanyika katika kata ya Nyakato ndani ta Manispaa hiyo.

“Haiwezekani hata siku moja Mkuu wa Wilaya anayeteuliwa na Rais ambaye naye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilya kuhudhuria Mkutano wa Chadema wakati yeye ni mwanachama wa CCM napenda niwaambie hiyo haipo na haitatokea kwa Viongozi kama hao kuhudhuria mikutano ya vyama vya upinzani,”alisema.

Alitumia nafasi hiyo kuwaomba Viongozi wa vyama vya siasa kuacha tabia ya kupanda jukwaa na kuanza kumtukana Rais Jakaya Kikwete na kusema kuwa wameshachoka na matusi hao na kuomba jeshi la polisi kwa kiongozi yeyote atakayetumia jukwaa kuktusi rais achukuliwe hatua pamoja na kufikishwa mahakamani.

“Sisi watanzania hatua utamaduni huu wa kijana au mtu kumtukana mzazi wake Rasi ni amir Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama hapaswi hata siku moja kumtukana hii ni kumkosea adabu na tunapenda kuwaambia jeshi la polisi kuwakamata wote wenye mchezo huu na kuwafikisha mahakamani,”alisema.

Alisema kuwa CCM imekuwa ikitumia majukwaa ya siasa hasa mikutano ya Siasa kwa ajoili ya kurekebisha mapungufu ambayo yanaonekana na wapinzani kitu ambacho kinaendelea kushika hatamu ya uongozi nchini.


Mwisho
Read More...

Monday, December 10, 2012

WAZEE WA MUSOMA WANG'AKA

 *Wataka mwandishi aliyeandika habari hiyo akamatwe
 *Siasa zaharibu Manispaa hiyo
 *Kaimu kamanda wa Polisi katika wilaya hiyo Lucas Hupa asema  matukio yaliyoripotiwa ni matatu na sio ya kuchinjwa
 
 
 
 Wachungaji wa Makanisa mbalimbali Manispaa ya Musoma, Mkoa wa Mara wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo, Jackson Msome (hayupo Pichani) baada ya Wazee, viongozi, Mashehe na Wachungaji kukanusha habari za watu 17 kuchinjwa.
 Wazee wa Manispaa ya Musoma wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Jackson Msome (Hayupo Pichani) baada ya wazee hao kupinga vikali taarifa zilizochapishwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari na kutangazwa kuwa watu 17 wachinjwa Musoma.
 Wazee waliofurika katika ukumbi wa Chuo cha Waganga Manispaa ya Musoma waliojitokeza kwa ajili ya kupinga habari za upotoshaji na uzushi zilizotangazwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini kuwa watu 17 wachinjwa musoma.
 Mkuu wa Wilaya Jackson Msome akisoma gazeti la Mtanzania ambalo hivi karibuni lenye kichwa cha habari Watu wachinjwa Musoma. Ambapo wananchi wa Manispaa hiyo kuingiwa na hofu na kusababisha baadhi ya wanafunzi kugoma kwenda shuleni kuogopa kuchinjwa. 
 Mkuu wa Wilaya ya Musoma Jackson Msome Akizungumza jambo mbele ya Wazee, Viongozi Mbalimbali, Mashehe na wachungaji (Hawapo Pichani) wakati akizungumza nao kwenye ukumbi wa Chuo cha waganga Manispaa hiyo.
 Katibu wa NCCR Mageuzi Mkoa wa Mara Tabu Said akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Musoma Jackson Msome wakati akizungumza na wazee, viongozi, wachungaji na mashehe hivi karibuni.
 
 
 
Na Thomas Dominick,
Musoma

WAZEE, Viongozi wa vyama vya Siasa na Serikali, Wachungaji na Mashehe Wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara wamekanusha vikali taarifa zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti na Televisheni nchini kuwa ndani ya wilaya hiyo watu 17 wakiwemo wanawake 5 wamechinjwa kati ya Oktoba hadi Desemba mwaka huu.

Wazee hao pia waliiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo kumkamata mwandishi wa habari hizo ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria kutoa ushahidi wa watu waliochinjwa kisha kumfikisha mahakamani kujibu mashitaka ya kuandika habari za uzushi na uchochezi na kuwatia hofu wananchi.

Wakizungumza na Mkuu wa Wilaya hiyo Jackson Msome na kamati yake ulinzi na usalama kwenye kikao cha dharura kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Waganga katika Manispaa hiyo wazee hao kwa kauli moja walimuhakikishi Mkuu wa wilaya hiyo kuwa habari hizo ni za uzushi zenye kuwatia hofu wananchi.

“Ukisoma kwenye haya magazeti utagundua habari hii imekaa kisiasa kwani hata Mbunge wa Chadema Vicent Nyerere anadiriki kusema kuwa anamtaka IGP said Mwema akomeshe mauaji hayo pia kamati ya ulinzi na usalama imekalia siasa huu ni uzushi na tunapinga kama kuna ukweli tunaomba otoe ushahidi kwa kuonyesha maiti zilizochinjwa,”alisema Mzee Seleman Kerenge.

Alisema kuwa vyombo hivyo vya habari vinalengo vya kuvuruga hali halisi ya amani na usalama ndani ya mji wa Musoma na kudai kuwa hakuna mtu yeyote aliwahi kuchinjwa ndani ya Manispaa hiyo.

Mzee Abdu Husein wa Makoko alisema kuwa wazazi wengi nchini hawapendi kutoa matatizo ya watoto wao hata kama wanashiriki katika vitendo viovu ambapo wanazua matatizo makubwa kwenye jamii.

“Tuna mapungufu makubwa sisi kama wazazi hata kama unajua matatizo ya vijana wako hutaki kusema ukweli, wazazi wengi hata vikao na vijana wao hawafanyi, tuna mamlaka lakini hatuyatumii,”alisema Husein kwa hasira kubwa.

Akitoa taarifa mbele ya wazee na mkuu wa wilaya Kaimu kamanda wa Polisi katika wilaya hiyo Lucas Hupa alisema kuwa matukio ambayo yalitokea katika kipindi cha mwezi Oktoba na Novemba ni matatu.

Alisema kuwa tukio la kwanza lilitokea Oktoba 19, Enock ambaye
alikuwa mlinzi alifariki dunia katika Hospitali ya Mkoa wa Mara baada ya kukatwa kwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa majambazi.

Tukio la pili lilitokea Oktoba 28, mwaka huu ambapo Msichana Lilian Bonifance (12) aliuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kutupwa na tukio la mwisho lilitokea Novemba 21 ambapo mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya Salama aliuawa na watu wanaodai kuwa majambazi.

Hupa alisema kuwa tayari jeshi hilo linawashikilia watu 16 na
watuhumiwa nane walisomewa mashitaka ya mauaji na kupelekwa magereza.

Naye Mkuu wa Wilaya Msome alisema kuwa kuna matukio yapo ndani ya wilaya hiyo lakini sio kama inavyozungumzwa kwa sasa ambapo ni hali ya kuwatisha wananchi wa Manispaa hiyo.

“Waandishi wa habari ni ndugu zetu wote tunafanya kazi kwa kuwatumikia wananchi tuache kuandika habari za uzushi na uchochezi ambazo zinatia hofu wananchi wetu,”alisema Msome.

Msome alisema kuwa Waandishi wa habari hawajaitendea haki Manispaa hiyo kutokana na habari hiyo ambayo alisema kuwa ni ya uzushi na kuwaomba kuandika habari sahihi ambazo hazipotoshi umma.

“Madhumuni ya vyombo vya habari na kazi ya mwandishi wa habari ni kufundisha, kuburudisha na kuelimisha sio kupotosha na kuchochea hayo sio maaili ya uandishi wa habari,”alisema.

Baada ya ukanushaji wa mauaji hayo Msome amewaomba wazee, Viongozi naViongozi wa dini kushirikiana na kuanzisha ulinzi shirikishi ili kuepukana na uzushi kama huo uliotokea ambapo ataanza na mafunzo juu ya ulinzi huo ambao yataanza Desemba 13 mwaka huu kwa kata nne za Iringo, Mkendo, Kitaji na na zingine zitafuata.

Taarifa ambazo hivi karibuni zilitolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa
Mara kupitia kwa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu kuwa ni matukio mawili ya watu kuchinjwa ndiyo yaliyoripotiwa na yalitokea katika Wilaya ya Butiama na sio watu 17 kama ilivyotangazwa.

Tukio la kwanza ni mwanawake aliyetambulika kwa jina la Blandina Peru (28) mkazi wa kijiji cha Mahare, kata ya Etaro aliuwawa Desemba 2 mwaka huu kwa kukatwa koromeo na kubakwa na wauaji kabla ya kumuua wakati akiwa porini akikata kuni na watuhumiwa wa tukio hilo bado hawajakamatwa.

Tukio la pili lilitokea Kijiji cha Kabegi, Kata ya Nyakatende, Wilaya
hiyo hiyo ambapo Sabina Mkireri (44) mkazi wa kijiji cha kiemba
aliwawa kwa kuchinjwa shingo na kichwa chake kuchukuliwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha kabegi na watu sita wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.

MWISHO.
Read More...

Friday, December 7, 2012

POLISI MARA YAKANUSHA UVUMI WA WATU 15 MKOANI HUMO KUCHINJWA.


Baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoa Mara wakiwa ndani ya ofisi ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu wakisubiria taarifa muhimu juu ya uvumi ulioenea nchi nzima wa mauaji wa wananchi wa mkoa huo. 


 Mwandishi Mkongwe Mkoani Mara Maxmilian Ngesi (mwenye shati la njano) akisoma meseji kwenye simu yake anayetazamana naye ni Shomari Binda na anayechukua picha za video ni Dick Mohamed mwakilishi wa Star TV Mkoani hapo wakati akiwa ndani ya ofisi ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu.

 
 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya taarifa za uzushi zilizozagaa nchi nzima kwa kusambazwa kwa wananchi wa mkoa huo pamoja na vyombo vya habari kuwa zaidi ya watu 15 wamechinjwa na vichwa vyao kuchukuliwa na watu wasiojulikana.

*watakaobainika kusambaza uongo huo kukiona
*waandishi wa habari wapashwa 

Na Thomas Dominick,
Mara

Jeshi la Polisi Mkoani Mara limekanusha uvumi wa kutishia wananchi toka baadhi  wananchi wenye nia mbaya na vyombo vya habari nchini kutangaza na kusambaza kuwa ndani ya mwezi mmoja watu 15 wameuwawa kwa kuchinjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalumu ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu alisema kuwa kumekua na uvumi kuwa katika Mkoa wa huo wananchi wamekuwa wakichinjwa na tayari watu 15 wameuwawa kwa kuchinjwa kitu ambacho ni uongo.

Kamanda Lusingu alisema kutokana na uvumi huo wamekua wakipokea simu toka kwa wananchi na viongozi ndani ya Manspaa ya Musoma katika kata ya nyakato kwamba kuna mwanafunzi ameonekana ameuwawa kwa kukatwa kichwa katika makaburi ya Musoma bus na jeshi la polisi likifuatilia wanakuta ni taarifa za uongo na za kuwatisha wananchi.

Alisema kuwa matukio mawili ndiyo yaliyoripotiwa ambapo wanawake wawili waliuawa  kati yao ni Blandina Peru (28) mkazi wa kijiji cha Mahare, kata ya Etaro ambapo aliuwawa Desemba 2 mwaka huu kwa kukatwa koromeo na kubakwa na wauaji kabla ya kumuua wakati akiwa porini akikata kuni na watuhumiwa wa tukio hilo bado hawajakamatwa.

Tukio la pili lilitokea Kabegi kata ya Nyakatende wilayani butiama ambapo Sabina Mkireri (44) mkazi wa kijiji cha kiemba aliwawa kwa kuchinjwa shingo na kichwa chake kuchukuliwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha kabegi na watu sita wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.

Kutokana na uvumi huo amewatoa hofu wananchi  juu ya mauaji hayo na kuwatahadharisha akina mama hasa maeneo ya vijijini wanapokua katika shughuli zao za kilimo na utafutaji wa kuni wawe waangalifu na watoe taarifa mapema wanaposhuku jambo lolote lisilo lakawaida.

“Nachukua nafasi hii kuwatoa hofu wananchi juu ya uvumi uliozagaa wa mauaji hayo na nawatahadharisha akina mama hasa maeneo ya vijijini wanapokua katika shughuli zao za kilimo na utafutaji wa kuni wawe waangalifu na watoe taarifa mapema wanaposhuku jambo lolote lisilo la kawaida,”alisema Lusingu.

Kwa upande mwingine Jeshi hilo limewaomba waandishi wa habari kupata taarifa kutoka kwenye vyanzo husika pia kwa watu ambao wanaoanzisha uvumi wakibainika wanatoa habari za uvumi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Aliongeza kuwa kwa sasa wanaendelea na msako maeneo mbalimbali ya manispaa ya Musoma na wilaya ya butiama ambapo kuna watu watano wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kwa makosa yakupatikana na pombe haramu ya gongo na wengine wanashikiliwa kwa kupatikana na bangi na wote watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Mwisho


 


Read More...