Baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoa Mara wakiwa ndani ya ofisi ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu wakisubiria taarifa muhimu juu ya uvumi ulioenea nchi nzima wa mauaji wa wananchi wa mkoa huo.
Mwandishi Mkongwe Mkoani Mara Maxmilian Ngesi (mwenye shati la njano) akisoma meseji kwenye simu yake anayetazamana naye ni Shomari Binda na anayechukua picha za video ni Dick Mohamed mwakilishi wa Star TV Mkoani hapo wakati akiwa ndani ya ofisi ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya taarifa za uzushi zilizozagaa nchi nzima kwa kusambazwa kwa wananchi wa mkoa huo pamoja na vyombo vya habari kuwa zaidi ya watu 15 wamechinjwa na vichwa vyao kuchukuliwa na watu wasiojulikana.
*watakaobainika kusambaza uongo huo kukiona
*waandishi wa habari wapashwa
Na Thomas Dominick,
Mara
Jeshi la Polisi Mkoani Mara limekanusha uvumi wa kutishia
wananchi toka baadhi wananchi wenye nia mbaya na vyombo vya habari nchini kutangaza na kusambaza kuwa ndani ya mwezi mmoja watu
15 wameuwawa kwa kuchinjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalumu
ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu
alisema kuwa kumekua na uvumi kuwa katika Mkoa wa huo wananchi wamekuwa
wakichinjwa na tayari watu 15 wameuwawa kwa kuchinjwa kitu ambacho ni uongo.
Kamanda Lusingu alisema kutokana na uvumi huo wamekua
wakipokea simu toka kwa wananchi na viongozi ndani ya Manspaa ya Musoma katika
kata ya nyakato kwamba kuna mwanafunzi ameonekana ameuwawa kwa kukatwa kichwa
katika makaburi ya Musoma bus na jeshi la polisi likifuatilia wanakuta ni
taarifa za uongo na za kuwatisha wananchi.
Alisema kuwa matukio mawili ndiyo yaliyoripotiwa ambapo wanawake
wawili waliuawa kati yao ni Blandina
Peru (28) mkazi wa kijiji cha Mahare, kata ya Etaro ambapo aliuwawa Desemba 2
mwaka huu kwa kukatwa koromeo na kubakwa na wauaji kabla ya kumuua wakati akiwa
porini akikata kuni na watuhumiwa wa tukio hilo bado hawajakamatwa.
Tukio la pili lilitokea Kabegi kata ya Nyakatende wilayani
butiama ambapo Sabina Mkireri (44) mkazi wa kijiji cha kiemba aliwawa kwa
kuchinjwa shingo na kichwa chake kuchukuliwa na watu wasiojulikana katika
kijiji cha kabegi na watu sita wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.
Kutokana na uvumi huo amewatoa hofu wananchi juu ya mauaji hayo na kuwatahadharisha akina
mama hasa maeneo ya vijijini wanapokua katika shughuli zao za kilimo na
utafutaji wa kuni wawe waangalifu na watoe taarifa mapema wanaposhuku jambo
lolote lisilo lakawaida.
“Nachukua nafasi hii kuwatoa hofu wananchi juu ya uvumi
uliozagaa wa mauaji hayo na nawatahadharisha akina mama hasa maeneo ya vijijini
wanapokua katika shughuli zao za kilimo na utafutaji wa kuni wawe waangalifu na
watoe taarifa mapema wanaposhuku jambo lolote lisilo la kawaida,”alisema
Lusingu.
Kwa upande mwingine Jeshi hilo limewaomba waandishi wa
habari kupata taarifa kutoka kwenye vyanzo husika pia kwa watu ambao
wanaoanzisha uvumi wakibainika wanatoa habari za uvumi hatua za kisheria zitachukuliwa
dhidi yao.
Aliongeza kuwa kwa sasa wanaendelea na msako maeneo
mbalimbali ya manispaa ya Musoma na wilaya ya butiama ambapo kuna watu watano
wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kwa makosa yakupatikana na pombe haramu ya
gongo na wengine wanashikiliwa kwa kupatikana na bangi na wote watafikishwa
mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment