Sunday, December 2, 2012

WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA KUWA MGENI RASMI SIKU YA WATU WENYE ULEMAVU KITAIFA ITAFANYIKA MKOANI MARA.

 Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Clement Lujaji (mwenye suti nyeusi) akizungumza jambo fulani wakati akizungumza na wajumbe wa kamati ya siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani pamoja na waandishi wa habari (Hawapo Pichani) maadhimisho hayo yatafanyika Desemba 3, mwaka huu katika uwanja wa Karume Manispaa ya Musoma.
Na Thomas Dominick,
Musoma

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemevu Duniani ambapo Kitaifa yatafanyika Mkoani Mara Desemba 3 mwaka huu.

Maadhimisho ya siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani yanatokana na tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa azimio namba 47/3 la mwaka 1992.

Akizungumza na vyombo vya habari Katibu Tawala wa Mkoa huo, Clement Lujaji alisema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika katika kiwanja cha Karume manispaa ya Musoma.

Alisema kuwa siku siku ya watu wenye ulemavu Duniani kufanyika Desemba 3 kila mwaka inalenga kuhamasisha jamii katika nchi husika kutambua haki na fursa sawa ushiriki wa watu wenye ulemavu katika masuala ya maendeleo.

“Kutambua mahitaji yao na changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kukabiliana nazo,”alisema Lujaji.

Alisema kuwa maadhimisho hayo yameanza Desemba Mosi mwaka huu ambapo wamefungua kituo cha walemavu (CBR) katika Kijiji cha Nyabange Musoma vijijini na Desemba 2 kutafanyika mashindano ya michezo ipatayo 12.

"Siku ya kilele tutatoa tuzo kwa mshindi wa mashindano hayo pamoja na kusikiliza hotuba kutoka kwa mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda,"alisema.

Lujaji amewaomba wananchi wa Mkoa huo kuungana na walemavu katika maadhimisho hayo ambapo kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka katika Halmashauri zote sita za Mkoa huo.


Mwisho

0 comments:

Post a Comment