Saturday, December 22, 2012

MAUAJI MENGINE YATOKEA BUTIAMA MKOANI MARA





Na Thomas Dominick,
Butiama

MATUKIO ya kutisha ya kuchinjwa watu na kuondoka na vichwa wanaendelea kushamiri Wilayani Butiama Mkoa wa Mara Baada ya Mwanamke mwingine aliyejulikana kwa jina Tabu Makanya (68) Mkazi wa Kijiji cha Kwikuba kuuawa na watu wanne ambapo sasa idadi imefikia watu wanne wakiwepo wanawake watatu.

Mauaji hayo yalitokea yalitokea Desemba 21, mwaka huu saa 5:30 usiku ambapo wauaji hao walifika nyumbani kwa marehemu na kumshambulia kwa kumpiga na fimbo na bapa za panga sehemu mbalimbali ili kumlegeza mwili wake na baadaye kumchinja na kuchukua kichwa chake ambapo waliweka kwenye mfuko wa salphet.

Kutokana na kufuatana kwa matukio hayo wananchi na waendesha Pikipki waliandamana na kufika kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Absalom Mwakyoma ambapo aliwatuliza kisha kutawanyika na kurudi Hospitali ya Mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo Absalom Mwakyoma alisema kuwa wauaji hao wanajulikana lakini majina yao yamehifadhiwa hadi watakapokamatwa.

"Baada ya kuondoka kwa wauaji hao nyumbani kwa marehemu ndipo vijana waliopo kwenye nyumba hiyo uwani pamoja na majirani walipiga yowe na kuanza kuwafukuza na baada ya kuona wanazidiwa walikitupa kichwa hicho na kutokomea gizani kwenye vichaka,"alisema Mwakyoma.

Kamanda Mwakyoma alisema kuwa juhudi za kufuatilia wahusika zimeanza kwa nguvu zote mara tu baada ya tukio hilo kutokea lakini hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa.

Matukio hayo ya watu kuchinjwa Wilayani Butiama yamefikia manne hadi sasa ambapo Desemba 2, Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Blandina Peru alichinjwa na kuchukuliwa damu yake tu, ambapo watuhumiwa watatu wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.

"Katika tukio hili tuliwakamata watuhumiwa watatu na wameshakiri kuhusika na tukio hilo na majina yao ni Sura Siriro, Jani Magesa na Mgasa Nyarukama na tukio la Sabina Mkireri wa kijiji cha Kabegi, Kata ya Nyakatende wilayani humo watu sita wamekamatwa na wanahojiwa kuhusiana na tukio hilo,"alisema.

Tukio jingine ni la mwendesha Pikipiki maarufu Bodaboda Thomas Majengo ambaye ni Mkazi wa Kiara Manispaa ya Musoma alichinjwa kisha kunyang'anywa pikipiki hiyo.

Kamanda Mwakyoma alisema kuwa tukio lililofanywa na waendeshwa Pikipiki waliofika katika ofisi yake kwa ajili ya kuomba kuonana naye walikuwa wameagizwa maalumu kutokana na kukanusha idadi ya watu waliotangazwa kuuawa ya watu 17.

"Ninasema kuwa mtu yeyote ambaye atahamasisha watu kuandamana na kuvamia ofisi na kufanya vurugu hatasalimika mkono wa sheria lazima utampitia,"alisema.

Alisema kuwa wananchi wanatakiwa kutii sheria bila shuruti na yeyote atakaye jitokeza kwa ajili ya vurugu jeshi hilo halitajali anafanya kazi katika taasisi gani na kudai kuwa jeshi hilo halitaki kusuguana na wanasiasa kwani kusema jambo lolote ni haki yao na wapo kwenye uwanja wao.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment