Tuesday, February 12, 2013

MCHUNGAJI AKANUSHA VIKALI TAARIFA ZILIZOTOLEWA NA RADIO FREE AFRICA



Baadhi ya Waandishi wa habari wa Mkoa wa Mara wakiwa katika chumba cha mchungaji Daudi Makoye kwa ajili ya kwenda kusikilza wito walioitiwa na mchungaji huyo.

MWENYEKITI wa Kanisa la Waadventista wasabato Jimbo la Mara na Ukerewe (Mara Conference), Daudi Makoye amekanusha vikali mbele ya waandishi wa habari taarifa  iliyotolewa na Radio  Free Africa kuwa Mchungaji wa Kanisa hilo la Ukerewe, Emmanuel Tarara kuwa amebaka mtoto mwenye umri wa miaka minane na kwamba huyo si mchungaji wa kanisa hilo.


 
Na Thomas Dominick,
Musoma.

MWENYEKITI wa Kanisa la Waadventista wasabato Jimbo la Mara na Ukerewe (Mara Conference), Daudi Makoye amekanusha vikali taarifa  iliyotolewa na Radio  Free Africa kuwa Mchungaji wa Kanisa la Waadvetista wa Sabato la Ukerewe, Emmanuel Tarara kuwa amebaka mtoto mwenye umri wa miaka minane na kwamba huyo si mchungaji wa kanisa hilo.

Sambamba na kumtaka mtangazaji wa redio hiyo Jovinta Kaijage kukanusha mara moja na kuomba radhi kwa kanisa hilo na watanzania kwa ujumla la sivyo watamchukulia hatua yeye na chombo chake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Kanisa la waadventisa wa sabato la Kamunyonge,  Mchungaji Makoye  alisema kuwa taarifa hiyo iliyotangazwa juzi katika kipindi chake cha “Matukio” kinachotangazwa kuanzia saa moja ya asubuhi, ilitangazwa na mwandishi wake Jovinta Kaijage kutoka Ukerewe.


"Tunapenda kukanusha vikali taarifa hii kwa sababu hauna ukweli wowote Kanisa la Waadventista Wasabato kwa sasa ina wachungaji watatu katika wilaya ya Ukerewe.”alisema Mchungaji Makoye.

Aliwataja wachungaji wa Ukerewe ni pamoja na Mchungaji Elifamili Kashanga anayesimamia mtaa wa Mrutunguru, Mchungaji Kapete Mafuru anayesimamia mtaa wa Ilangara.

Mitaa mingine inasimamiwa na Mchungaji Zefa Ayugi anayesimamia mtaa wa Buhima na mtaa wa Nansio unasimamiwa na Mzee wa kanisa ndugu Staford Maiga anayekaimu nafasi ya mchungaji Daniel Muhono aliyehamia Mtaa wa Buturi hadi atakapopelekwa  mchungaji mwingine. 

Alisema kuwa kutokana na taarifa hizo waliwasiliana na Mzee wa kanisa, Staford Maiga wa Nansio ambaye walizungumza nae kwa simu juu ya jina hilo na kuthibitisha kuwa  Emmanuel Tarara hata si mshiriki wa kanisa hilo.

Aidha amewaomba  waandishi wa habari na hasa wa chombo kilihusika (RFA) kutoa taarifa sahihi iliyofanyiwa uchunguzi  na kuhakikishwa kisha kuutangaza kwa wananchi. 

“Waandishi wa habari ni watu waliiopewa  dhamana ya kuelemisha na kudumisha amani ya umma ya watanzania na kokote na kwamba  ni taarifa za uhakika tua nizo zinazosikika, hivyo  si vizuri kutoa taarifa isiyo sahihi na yenye malengo mbaya kwa  hisia za watu na inayoweza kuleta mfarakano na fitina katika jamii,”alisema.

Pia taarifa isitolewe ambayo inaweza kuleta picha mbaya au kupaka matope dhehebu na kuharibia sifa ya kanisa hivyo pamoja amemtaka Mwandishi huyo aombe radhi kwa jumuia ya kanisa la Waadventista Wasabato na watanzania wengine waliosikiliza habari hiyo  kurekebisha taarifa hiyo haraka.

MWISHO. 
Read More...

Thursday, February 7, 2013

MAUAJI MENGINE BUTIAMA, WANAJESHI WAZUIA MAAFA








 Gari ya Jeshi la Polisi likiwa linatokea eneo la tukio la mauaji kijiji cha Etaro ambapo walichukua mwili wa marehemu Magere Masatu na kuupeleka Hospitali ya Mkoa wa Mara.
 Askari wa kutuliza ghasia wa Mkoa wa Mara wakiwa katika eneo la tukio kuzuia ghasia kutoka kwa waendesha pikipiki na wananchi wa kijiji cha Etaro wilaya ya Butiama
 Wananchi wa Kijiji cha Etaro wakiangalia nyumba ya Magee Saganda iliyochomwa moto baada ya mtoto wake Koti Magee kudaiwa kuhusika katika mauaji ya mwendesha pikipiki.
 Baiskeli zikiwa zimeungua ndani ya nyumba ya mtuhumiwa wa mauaji ya kijana Magere Masatu.
 wananchi wa Etaro wakishangaa tukio la uchomaji wa moto nyumba ya kijana anayetuhumiwa tukio la mauaji.


Na Thomas Dominick,
Butiama

MAUAJI ya kutisha bado yanaendelea kutokea katika Wilaya ya Butiama, Mkoa wa Mara baada ya kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Magere Masatu Mkazi wa Mtaa wa Nyakato, Wilaya ya Musoma kuuawa kasha kutupwa kwenye Mto wenye maji.

Katika tukio hilo Wanajeshi waliingilia kati na walifanikiwa kudhibiti maafa zaidi baada ya nyumba moja ya mtuhumiwa wa mauaji hayo kuchoma moto na kuteketeza kila kitu.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wanadai kuwa tukio hilo lilitokea tarehe Februari 4 mwaka huu katika kijiji cha Etaro wilayani humo, ambapo walisema kuwa siku ya tukio marehemu aligongana na pikipiki na mwenzake ambaye akufahamika jina lake.

Walisema kuwa baada ya kugongana marehemu aliamua kumlipa fedha aliyegongana naye lakini balozi wa eneo la tukio alipelekewa pikipiki ya marehemu kwa ajili ya kuihifadhi.

“Baada ya tukio kweli pikipiki ilichukuliwa na kupelekwa kwa balozi wakati wanakwenda kuna vijana wawili walikuwa wakifuatilia kwa nyuma, na baada ya hapo marehemu hakuonekana tena hadi jana alipoonekana amekufa na yupo ndani ya mto,”alisema shuhuda aliyekataa kutaja jina lake.

Baada ya waendesha pikipiki wa Wilaya ya Musoma kupata taarifa kwa kuuwa kwa mwenzao walikwenda na kuvamia kijiji hicho kwa kuwapiga baadhi ya wananchi na balozi ambaye alikuwa amehifadhi pikipiki hiyo kisha kumtaja mmoja wa wauaji hao kuwa ni Koti Magee mkazi wa kijiji hicho.

Waendesha pikipiki hao walikwenda hadi kwa mtuhumiwa huyo na walimkuta lakini alifanikiwa kuwatoroka kisha kukimbilia ziwani na kujitosa kwenye maji kuogelea ikiwa ndio pona yake.

Baada ya kumkosa vijana hao walirudi nyumbani anapoishi kijana huyo ambaye anaishi na baba yake mzazi aliyejulikana kwa jina la Magee Saganda kisha kuitia moto nyumba moja na kuteketea kabisa.

Wanajeshi wa Jeshi la wananchi waliwahi kufika katika eneo la tukio na kuzuia uchomaji moto wa nyumba zingine ambazo nazo zilikuwa zinztaka kutiwa moto.

Mwandishi wa habari alifika katika eneo la tukio ambapo kwenye nyumba hiyo hapakuwepo na mtu yeyote yule lakini inadaiwa akina mama wa nyumba hiyo walipigwa na waendesha pikipiki hao na kukimbilia kusikojulikana.

Jeshi la polisi baada ya kufika lilichukua mwili wa marehemu na Balozi wa eneo hilo Peter Mabojano na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Mwili wa marehemu umepelekwa katika Hospitali ya Mkoa huo na umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Tukio hili ni la tano kutokea katika wilaya ya Butiama ambapo katika matukio ya kuanzia Novemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu ambapo matukio hayo ni kama ifuatavyo

Matukio hayo ni pamoja na la Desemba 21, mwaka huu saa 5:30 usiku Tabu Makanya (68) Mkazi wa Kijiji cha Kwikuba alichinjwa lakini watuhumiwa wakiwa katika harakati ya kuondoka na kichwa chake waliwahiwa na wananchi kisha kukitupa.

Lingine lilitokea Desemba 2,Blandina Peru alichinjwa na kuchukuliwa damu yake tu na Sabina Mkireri wa kijiji cha Kabegi, Kata alichinjwa na kuondoka na kichwa chake

Tukio jingine ni la kijana aliyetambuliwa kwa jina la Thomas Majengo (23-28) Mkazi wa Kiara Musoma Mjini alichijwa na kunyang'anywa pikipiki.


MWISHO





Read More...

Monday, February 4, 2013

IMANI ZA KISHIRIKINA ZAMTOA UHAI

Na Thomas Dominick,
Musoma


MKAZI mmoja wa kijiji cha Nyiberekere kilichopo Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara Nyabuke Maheri ,ameuawa kwa kupigwa mawe kisha kuchomwa moto kwa tuhuma za uchawi.

Kwa mujibu wa Taarifa kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Absalom Mwakyoma,Bibi huyo mwenye umri wa miaka 68 alifikwa na mauti Februari 2 majira ya saa 10 jioni baada ya watu kadhaa kufika nyumbani kwake na kuubwaga mwili wa mtu aliyedaiwa kuuawa kichawi na bibi huyo Februari 1.

Watu hao wanaoelezwa kuwa wa ukoo mmoja na bibi huyo waliamua kujichukulia sheria mkononi baada ya marehemu Nyabunke kuwajibu kuwa hata wakimsusia maiti hiyo hawana uwezo wa kumfanya lolote.

Kamanda Mwakyoma alifafanua kuwa,hata hivyo mwili wa marehemu Kitene Kasinde(50)ulizikwa jana (feb 3)baada ya viongozi wa eneo hilo na jeshi la polisi kushauriana na ndugu hao kuondoa tofauti zao kwa kutoamani dhana ya uchawi na badala yake washirikiane kuusiri mwili huo.

Akizungumzia tabia ya wananchi kujichukulia sheria mkonono Mwakyoma ameapa kuwashughulikia ipasavyo wale wote wanaoendeleza tabia hiyo na kutoa wito kwa wanancho kushirikiana na kutoa taarifa kwa polisi pindi waonapo matukio ya aina hiyo.


MWISHO
Read More...

MUSOMA YAPATA MAFANIKIO KIUCHUMI






 Waandishi wa habari Bigambo Jeje akipata kinywaji wakati wakisubiri mkutano wa waandishi wa habari na Mkuu wa Wilaya Musoma Jackson Msome pembeni ni mwandishi mwingine Fazel Janja.
 Mwakilishi wa Sahara Media Mkoa wa Mara, Dick Mohamed akiwa anawajibika wakati wa mkutano wa waandishi wa habari na Mkuu wa Wilaya Musoma Jackson Msome.
 Mwandishi wa Mtanzania Shomari Binda na Pascal Buya wakiwa katika mkutano wa waandishi wa habari na Mkuu wa Wilaya Musoma Jackson Msome. Aliyekuwa akiwaeleza mwananchi wa Wilaya hiyo mafanikio ya serikali ya awamu ya Nne tangu Novemba mwaka 2005 hadi Desemba 2012.
 Mkuu wa Wilaya ya Musoma Jackson Msome akisoma mafanikio yaliyopatikana katika Wilaya hiyo chini ya Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Na Thomas Dominick,
Musoma

MANISPAA ya Musoma Mkoa wa Mara imeongeza mapato ya ndani hadi kufikia Shilingi Bilioni 1.039 Desemba mwaka 2012 sawa na asilimia 184.98 ukilinganisha mapato yaliyopatikana Novemba mwaka 2005 yaliyokuwa sh. Milioni 364.836/=.

Akisoma taarifa ya mafanikio hayo Mkuu wa Wilaya hiyo, Jackson Msome mbele ya waandishi wa habari ofisni kwake alisema kuwa katika kipindi hicho Manispaaa hiyo imeongeza ruzuku toka serikali kuu hadi kufikia Bilioni 11.862 sawa na asilimia 316.94 ukulinganisha mwaka 2005 ambapo ruzuku ilikuwa sh. Billion 2.845.

Msome alisema kuwa kutokana na kipato hicho Manispaa hiyo ina lengo la kupunguza utitiri wa vyanzo vya mapato visivyo na tija ambavyo ni kero kwa wananchi na kuwa na vyanzo vichache vyenye tija.

“Manispaa yetu ina jumla ya vyanzo vya mapato 17 vya ndani na hii baada ya kupunguza vyanzo vya mapato visivyo na tija lakini tumeweza kupata mafanikio makubwa katika makusanyo yetu ya ndani,”alisema Msome.

Alisema kuwa kutokana na juhudi za Serikali pato la mkazi kwa mwaka limeongezeka katika kipindi hicho kutoka wastani wa shilingi 268,000/= mwaka 2005 hadi 602,000/= mwaka 2012 sawa na asilimia 225.

Alisema kuwa kupanda kwa pato hilo ni kutokana na wananchi wengi kujitokeza kufanya shughuli za ujasiriamali kwa kuchukua mikopo katika mashirika na taasisi za kifedha zilizopo ambapo idadi ya wanaofanya biashara rasmi wenye leseni wameongezeka kutoka 357 mwaka 2005 hadi 4659 mwaka 2012 sawa na asilimia 120.5.

Kwa upande wa afya zahanati zimeongezeka toka 15 mwaka 2005 hadi 22 mwaka 2012 kutokana na ufanisi wa utoaji wa huduma hiyo asilimia ya utoaji chanjo kimepanda toka 85 hadi 98 Desemba 2012.

“Aidha katika kuthibiti malaria serikali iligawa vyandarua kwa kaya zote kwa asilimia 100 pia madaktari na wauguzi wameongezeka toka 12 hadi 25 mwaka 2012, pamoja na mpango wa kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya rufaa ya Kwangwa umekamilika na shughuli zitaanza hivi karibuni,”alisema Msome.

mwisho

Read More...

Saturday, February 2, 2013

UNYAMA WAENDELEA MUSOMA MWINGINE ANYONGWA CHUPI YAOKOTWA PEMBENI YA MWILI WA MAREHEMU




 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Absalom Mwakyoma
 
Na Thomas Dominick,
Musoma

MTU mmoja ambaye jina lake halikufahamika mara moja mkazi wa Buhare Mgaranjabo, Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara alikutwa amekufa kwa kunyongwa na kanga shingoni na mwili wake kutupwa kichakani na watu wasiojulikana.

Taarifa liyotolewa kwa vyombo vya habari nchini na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Absalom Mwakyoma zilisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 31 mwaka huu saa 4:15 jioni.

Taarifa zinasema kuwa kando ya mwili wa marehemu ilikutwa chupi, skin tight zimechanwa, dumu la kuchotea maji likiwa mita 20 tokea mwili ulipokuwa.

Inadaiwa kuwa nywele za marehemu zilikutwa zikiwa zimefungwa kwenye kijiti kichakani hapo na kanga ikiwa shingoni huku ulimi wake ukiwa nje na kinyesi pembeni.

Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kuwabaini waliofanya tukio hilo ili sheria ichukue mkondo wake.

Mwakyoma ametoa wito kwa wananchi watakaokuwa na taarifa za watu au mtu waliohusika na mauaji hayo watoe kwa siri kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili wauaji hao wachukuliwe hatua za kisheria.

Matukio ya mauaji yamekuwa kero kwa wananchi wa Mkoa wa Mara ambapo Wilaya ya Butiama imeongoza kwa mauaji ya kikatili ambapo jumla ya watu wanne waliuawa katika kipindi cha Novemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu.
Read More...

Tuesday, January 15, 2013

PENGO KUBWA HOSPITALI YA MKOA WA MARA


                                                       Marehemu Daktari Joseph Nyamagirwa


Na Thomas Dominick
Musoma

DAKTARI Msaidizi Mkuu Daraja la kwanza wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara,Joseph Nyamagirwa (59)  amefariki Dunia juzi asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mkoa wa Mwanza kwa tatizo la uvimbe sehemu ya chini ya utumbo mpana.

Daktari huyo ameacha pengo kubwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara kutokana na kuwa tegemeo kubwa hasa kwa kutibu watoto na wanawake pamoja na upasuaji ambapo kwa sasa hospitali hiyo inahitaji madaktari 12 na hivi sasa waliopo ni watatu  tu.

Akitoa taarifa  ya kifo hicho,Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Iragi Ngerageza alisema kuwa Marehemu alikuwa na tatizo la tumbo ambalo alikuwa akilalamikia kuwa linauma ambapo Jan.8 Mwaka huu alifika Hospitalini hapa kwa matibabu ambayo iliwalazimu kumpeka katika hospitali ya Rufaa ya Bugando na siku hiyo hiyo akifanyiwa upasuaji wa kina.


Alisema kuwa pamoja na jitihada za madaktari bingwa kuokoa maisha yake lakini hali yake iliendelea kuzorota na hatimaye mauti kumfika Jan. 14 mwaka huu asubuhi ambapo alikuwa amelazwa katika chumba cha upasuaji idara ya upasuaji (Surgical Department) chumba namba 6 C 607.


Alikielezea sifa za marehemu alisema kuwa ni Daktari pekee ambaye alikuwa akifanya kazi kwa kujituma na kwa bidii kubwa na hata kama yuko likizo ataitwa kufanya kazi atakuja haraka na kwa gharama zake kusaidia wagonjwa ambao wanakuwa na hali mbaya.


“Kwa kweli Mkoa wa Mara tumepata pengo kubwa kumpoteza ambapo marehemu aliitwa jina la utani la ‘Chief’kutokana na uchapakazi wake,alikuwa alikifanya kazi ya uhakika kwa kuwa alikuwa atayari na uzoefu wa muda mrefu na kila upasuaji unapofanyika lazima awepo akimabatana na jopo la madaktari wengine kusaidiana nao na hatimaye kuokoa maisha ya wagonjwa wengi hasa akina Mama Wajawazito na Watoto”Alisema Ngerageza.


Aidha ametoa wito kwa Wizara ya afya kuangalia uwezekano wa kuleta madaktari kwani kuna upungufu mkubwa ambapo  kwa upande wa madaktari bigwa wanahitajika sita waliopo ni wawili tu na madaktari wasaidizi wanahitajika 28 waliopo ni 16 wamebaki 15.

Akizungumzia elimu yake Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara,Faustin Bigambo alisema,alimaliza elimu ya Sekondari mwaka 1976 katika Shule ya Sekondari ya Sengerema na kujiunga na Chuo cha Utabibu cha Tanga na baadae kujiendeleza katika Chuo cha Madaktari wasaidizi cha Bugando Mwanza(BMC).

Marehemu atazikwa Januari 17 mwaka huu kijijini kwao Butata Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara,ambapo Maziko hayo yanatarajiwa kuhuduhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,John Tuppa.
Read More...