Tuesday, November 27, 2012

JESHI LA POLISI LAVAMIA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA





Wanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake wakiwa na mabango kwa ajili ya kuanza maandamano katika kampeni ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake iliyofanyika katika Kijiji cha Kitasakwa Kata ya Bwiregi Wilayani Butiama iliyoandaliwa na Shirika la kutetea Haki za Wanawake na Watoto la ABCFoundation Chini ya Ufadhiri wa Shirika la (WILDAF).
 Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Absalom Mwakyoma akipokea maandamano (hawapo Pichani) katika kampeni ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake iliyofanyika katika Kijiji cha Kitasakwa Kata ya Bwiregi Wilayani Butiama.

Na Thomas Dominick,
Butiama,

JUMLA ya matukio 201 ya ukatili wa Kijinsia yamelipotiwa katika Jeshi la Polisi Mkoani Mara kutokea  maeneo mbalimbali ya Mkoa huo katika kipindi cha mwezi Januari hadi Novemba Mwaka huu huku jamii ikitakiwa kubadilika na kukomesha matukio ya namna hiyo kuendelea kutokea katika Jamii.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamanda wa Polisi Mkoani Mara Kamishina
Msaidizi Mwandamizi Absalom Mwakyoma alipokuwa akifungua kampeni ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake iliyofanyika katika Kijiji cha Kitasakwa Kata ya Bwiregi Wilayani Butiama iliyoandaliwa na Shirika la kutetea Haki za Wanawake na Watoto la ABC Foundation Chini ya Ufadhiri wa Shirika la (WILDAF).

Alisema idadi hiyo imeongezeka tofauti na mwaka uliopita ambapo katika kipindi cha Mwaka jana matukio ya ukatili yaliyolipotiwa yalikuwa 148 huku watuhumiwa 51 walifikishwa Mahakamani na kati ya hao watuhumiwa 10 tayari wamekwisha hukumiwa na wanatumikia adhabu zao gerezani.

Alidai Mwanamke ni mtu ambaye anachangia kwa kiasi kikubwa katika Maendeleo ya Kijamii ikiwemo kuchangia shughuli za Kiuchumi katika Jamii pamoja na kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza Elimu kwa Watoto kwa kuwa wao kwa asilimia kubwa ndio wanaokuwa nao karibu hivyo anastahili kuheshimiwa na kupewa haki stahili.

Kamanda Mwakyoma alieleza kuwa Binadamu wote ni sawa na wanastahili kutambuliwa na kuheshimiwa utu wao hivyo ni wazi kwamba watu wote hususani Wanawake ambao wamekuwa wakinyanyaswa kutokana na jinsia zao ni ukiukwaji wa katiba ya Nchi na misingi ya Haki za Binadamu pale wanapofanyiwa ukatili.

Alisema Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia kwa kushirikiana na
Asasi mbalimbali zinazopambana na masuala ya ukatili wa kijinsia
watahakikisha mapambano ya kukomesha ukatili wa kijinsia Mkoani Mara yanakomeshwa hususani kwa Wanawake na Watoto wanaofanyiwa Ukeketaji.

“Nimeajiliwa kwa kufanya kazi na nitahakikisha nawashughulikia kwa mujibu wa Sheria wale wote ambao bado wanaendeleza matukio ya unyanyasaji kwa Wanawake na Watoto pale watakapobainika na sasa ni wajibu wa kila Mwananchi kubadilika na kuachana na masuala hayo.

“Lazima Mwanamke aheshimiwe na kila mmoja tusione ajabu leo kumuona Kamanda wa Polisi akiwa mgeni rasmi katika uzinduzi huu kwa maana sasa tumeamua kwa dhati kushirikiana na jamii katika masuala yote likiwemo suala la kupinga na kukomesha unyanyasaji wa kijinsia na ndio iliyopelekea Mwaka 2007 ukaanzishwa mtandao wa Polisi Wanawake na baadae Mwaka 2009 likaanzishwa dawati la jinsia la Wanawake na Watoto,”alisema Kamanda Mwakyoma.

Awali katika uzinduzi huo wa siku 16 za kupinga ukatili wa
Kijinsia,Mkuu wa Wilaya ya Butiama Angelina Mabula aliwataka Wanawake kutokuogopa kutoa taarifa zinazohusiana na masuala ya ukatili wa Kijinsia ili kila mmoja anaye husika aweze kufikishwa katika vyombo vya Sheria ili hatua dhidi yao ziweze kuchukuliwa.

Alisema inahitajika mikakati madhubuti zaidi kwa lengo la kuondoa
masuala ya ukatili wa kijinsia kwani pamoja na kuwepo Sheria za kuzuia masuala ya ukatili bado kumekuwepo na matukio kama hayo na kuwa kikwazo katika Maendeleo ya Wanawake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la ABC Foundation, Eustance Nyarugenda alilishukuru Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF) Kupitia Shirika la Kivulini kwa  ufadhiri wa siku hizo 16 za kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na kuahidi kuendelea na mapambano dhidi ua ukatili hata baada ya kumalizika kwa siku hizo.

0 comments:

Post a Comment