Wednesday, November 21, 2012

MUME AMPIGA MKEWE HADI KUPOTEZA FAHAMU KISA SIMU YA MKONONI






Mwanamke Pendo Malima aliyepigwa na mume wake hadi kupoteza fahamu kwa siku tatu akiwa katika Hospitali ya Mkoa wa mara alikolazwa kwa ajili ya kupatiwa Matibabu.

*Kisa cha Kupata Kipigo ni simu yake ya Mkononi
*Polisi wamsaka Mtuhumiwa ili akutane na mkono wa sheria
*Asema akitoka Hospitali harudi tena kwa Mume wake
 Habari zaidi ingia www.habarimotomotomara.blogspot.com
Na Thomas Dominick,
Musoma

Mwanamke aitwaye Pendo Malima (31) Mkazi wa Bohare Manispaa ya Musoma, Mkoani Mara alipoteza fahamu siku tatu baada ya kupigwa na Mumewe Ndege Aloyce ambaye ni Mvuvi kisa simu ya Mkononi.

Akizungumza na Habari Moto Moto Mara jana, Katika Hospitali ya Mkoa huo wodi namba 4 alipolazwa Pendo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 17 mwaka huu usiku na kuongeza kuwa mume wake huyo amekuwa na kawaida ya kumpiga wastani ya mara tatu kwa mwezi.

“Ni kawaida ya mume wangu kunipiga mara tatu kwa mwezi kwani yeye ndio mwanaume ndani ya nyumba na mimi nakubali na kuona ni kawaida yake,”alisema Pendo.

Alisema kuwa siku ya tukio mume wake alifika nyumbani usiku na kumuomba simu yake lakini mwanamke huyo alimuambia kuwa atampatia simu hiyo siku ya pili yake asubuhi.

“Baada ya kumjibu hivyo aliamua kunipiga hadi nilipopoteza fahamu na kutojua kilichoendelea hadi siku ya tatu ndipo nilipopata fahamu,”alisema Pendo.

Alisema kuwa aliolewa na mwanaume huyo tangu mwaka 1996 na waliishi maisha hayo ya kupigwa lakini walifanikiwa kupata watoto watatu ambapo mkubwa anaishi na bibi yake na wawili anaishi naye.

Pendo alisema kuwa kutokana na kipigo hicho ajajua hadi sasa wapi ameumia ingawa alidai kuwa kichwa kinamuuma ingawa kwa sasa anaendelea vizuri.

Alisema kuwa baada ya kupatiwa matibabu na kupona ataondoka kwenda kijijini kwao Kiemba wilayani Butiama kwa kuwa amechoshwa na maisha ya kupigwa.

Alisema kuwa walishatoa taarifa Polisi na jeshi hilo linamsaka mtuhumiwa ili aweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria ili achukuliwe hatua za kisheria pamoja na kufikishwa mahakamani.

Habari Moto Moto Mara ilifika ofisi ya kamanda wa Polisi Mkoa huo Absalom Mwakyoma ili kudhibitisha tukio hilo lakini hakupatikana kwa kuwa alikuwa kwenye kikao.

Mwisho



0 comments:

Post a Comment