Musoma
WATANZANIA wanne wamefanikiwa kutoroka katika kambi la mafunzo ya kijeshi nchini Ethiopia, kundi linalosadikiwa kuwa la Al Shabaab baada ya kurubuniwa na raia wa Somalia waliofika katika Kijiji cha Buhemba wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara kwa kuwaahidi wanawapeleka kwenye mgodi wa dhahabu nchini Ethiopia.
Inadaiwa kuwa watu hao walikwenda kijijini hapo wakiwa na mwenyeji wao aliyejulikana kwa jina moja la Nyambura mkazi wa Tarime ambaye alikuwa anafanya biashara ya kuchoma nyama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Chaku Maduhu Mkazi wa Bariadi Mkoa wa Simiyu ambaye ambaye alifanikiwa kutoroka alikuwa mchimbaji wa dhahabu katika mgodi wa Buhema alisema kuwa walikubaliana na watu hao kisha kuambatana nao kuelekea Tarime tayari kwa kuvuka mpaka kuingia nchini Kenya walikuwa na gari.
“Baada ya kufika mpakani yule mwenyeji wao alipatiwa fedha kiasi cha sh. Laki tano kasha kurudi Tarime hapo tulibadilisha gari na kuingia kwenye gari nyingine na kuvuka mpaka na kuanza safari ya kwenda Ethiopia,”alisema Maduhu.
Alisema kuwa walipofika nchini Kenya kijiji cha Myare ambayo ilikuwa kama kambi ya kukutana kisha walibadilishiwa usafiri na kupanda pikipiki kuelekea maporini kwa safari iliyochukua takribani masaa manne hadi kufika kambi iliyoandaliwa nchini Ethiopia.
“Tulipofika huko tulikutana na watanzania wengine ambao tayari walikuwa wameshatekwa kisha tuligawanishwa kwenye makundi na kupewa kibarua cha kuchimba madini,”alisema.
Alisema kuwa katika eneo hilo ambalo walikuwa wanachimba madini walikuwa wanakutana na mabaki ya risasi na mabomu alipowadadisi watanzania wenzake walidai kuwa msitu huo ni mwanzo kuna mistu mingine mbele.
“Niliamua kuwadadisi watanzania wenzangu walisema kuwa hapa ni mwanzo kuna msitu mwingine mbele ambako kuna mafunzo ya kijeshi ambapo nilijua kuwa hicho ni kikundi cha Al shabab cha nchini Somalia,”alisema.
Alisema kuwa watanzania wenzake walimuambia afanye kila liwezekanalo atoroke ili aweze kufikisha ujumbe kwa serikali ya Tanzania ili kuweza kuwasaidia watanzania hao kuwakwamua kwenye kundi hilo kwani wenzake walishindwa kutokana na afya zao kudhoofu .
“Mimi nilifanikiwa na wenzangu watatu kutoroka siku ambayo wasomali walikwenda kuabudu misikitini hiyo ndio ikawa nafasi yetu hadi nchini ambako tulikutana na mtanzania aliyetusaidia kuwasiliana na ndugu zetu ambao walitutumia nauli ya kurejea Tanzania,”alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma alipoyulizwa juu ya suala hilo alikiri kijana huyo alifanya mahojiano na mkuu wa upelelezi wa Mkoa huo Emmanuel Lukula na kusema kuwa wanalifanyia kazi suala hilo ili kupata ukweli wa jambo hilo.
“Tumelipokea lakini tunapenda kuwatahadharisha wananchi kuwa makini na wageni wanaoingia nchini ambao hawawajui na kuwarubuni,”alisema.
Amewataka wananchi wa Tanzania kuacha kuwa na tamaa ya utajiri wa haraka bali wafanye kazi kwa makini pia kutokubali kushawishiwa na watu wasiowajua ili kuepuka vitendo kama hivyo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment