Friday, February 22, 2013

CHADEMA MUSOMA YACHAFUKA MADIWANI WAFUKUZWA





  Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya  Meshack Rutantongani akisoma na kuelezea vifungu vya katiba ya CHADEMA baada ya kuamua kuwatimua madiwani wake wawili wa viti maalumu na Meya na wenzake wawili kupewa siku 14 kujieleza.

 Ofisi za chadema Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara

* Waliofukuzwa wasema hawatishiki 
* Wasema kilichofichwa kitafichuka 
* wadai zama za Chama zimefika mwisho
*Maslahi binafsi ndio chanzo cha mgogoro ndani ya chama hicho 

Na Thomas Dominick,
Musoma

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara kimewavua uanachama madiwani wawili wa viti maalumu na madiwani wengine watatu akiwemo Meya wa Manispaa Alex Kisurura kuandikiwa hati ya mashitaka na kutakiwa kujieleza  ndani ya siku 14 na baada ya hapo kikao kingine kitaitishwa kupitia maelezo yao ili hatua stahiki zichukuliwe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mwenezi wa Wilaya hiyo Meshack Rutantongani alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kwenye kikao cha kamati tendaji ya Wilaya kilichokaa Februari 21 mwaka huu na kufikia maamuzi hayo kutokana na utovu wa nidhamu wa madiwani hao.

“Chadema ni taasisi inayoendeshwa kwa katiba na kanuni zake ukisoma utakuta kuna mambo ambayo mwanachama au kiongozi hatakiwi kuyafanya kwa hivyo hawa wameenda kinyume na chama hivyo tumeamua wawili kuwafuta uanachama na hwo wengine wajieleze,”alisema Rutantongani.

Aliwataja madiwani wa viti maalumu waliovuliwa uanachama ni Habiba Ally na Miriam Daudi na waliondikiwa barua za kujieleza ni pamoja na meya Alex Kisurura ambaye pia ni diwani wa kata ya Nyamatare, Haile Siza Tarai diwani wa Kata ya kitaji na Angela Derrick diwani wa kata ya kamnyonge.

Alisema kuwa madiwani hao waliitwa kwenye kikao hicho lakini waligoma kuhudhuria ambapo hiyo nayo ni sehemu ya utovu wa nidhamu kwa kukataa wito wa kamati hiyo ambayo ni chombo kikubwa ndani ya chama hicho.

“Tumezingatia Kanuni za katiba ibara ya 5.66, 6.34 na 6.36 na tumefuata Ibara ya 11 kifungu cha I, II, III, IV, V, VI, VII, VIII, IX, X vyote hivyo vinazungumzia jinsi gani wanachama au kiongozi akifanya kosa hatua za kumchukulia,”alisema.

Alisema kuwa madiwani hao wamekuwa wakifanya makosa kwa kipindi kirefu na wamewahi kuitwa kwa ajili ya kujieleza pamoja na kupewa onyo lakini wamekuwa wakaidi na kurudia kufanya makosa.

Pia viongozi hao wamekuwa wakimpigia simu Katibu Mkuu Dr. Wilbroad kumuelezea mambo ya uongo kwa ajili ya kuwachonganisha naye kitendo ambacho wanadai kuwa kimewaudhi pia alisema kuwa pale wanapopigia simu Dr. Slaa anarudisha kwa viongozi hao.

Gazeti hili lilifanya mahojiano na baadhi ya madiwani hao ambapo Diwani wa kamnyonge angela Derrick alisema kuwa sababu ya kuandikiwa barua ya kujieleza kutokana na kutounga mkono mbinu yao ya kumuondoa Meya wa manispaa hiyo.

“Tunakubaliana, kwani wao sio waliotuleta hapa tumechaguliwa na kundi kubwa la wananchi na sio wao ambao wanataka maslahi yao binafsi yafanikiwe na hatupo kwenye chama kwa ajili ya kuendesha migogoro lakini hukumu ya shetani ni aibu, mungu atawaonyesha mambo yaliyojificha ndani ya chama na maslahi ambayo watu wanapigania kwa ajili ya kujinufaisha,”

“Mungu siku moja ataonyesha hukumu ya shetani na ukweli utaonekana kwa ubaya wao wanayotaka kuyatekeleza wananchi wawe wavumilivu kwa taarifa hizi lakini ukweli utafunuliwa,” alisema Angela.

Pia Diwani aliyevuliwa uanachama Habiba Ally hajui chochote anachoyambua kuwa ni Diwani halali wa  kwa kuwa hajapata barua kutoka kwenye chama.

“Hizo ni Propaganda zao tu kwa maslahi yao na kikundi kidogo ambacho kinataka maslahi yao yaimarike kutoka kwenye jasho la wananchi wa Musoma hivyo tumekuwa hatutaki kuwaunga ndio maana wanasema hatuna nidhamu ebu waulizeni ni kosa gani tumefanya kama watawapa majibu,”alisema Habiba.

Meya Alex Kisurura alisema kuwa hana taarifa ya kikao hicho na hajui kilifanyika lini kwa lengo gani lakini alisema kuwa mambo yanayotokea ndani ya Chadema ni kutokana na maslahi ya watu wachache ambao wanataka kujinufaisha kupitia kwenye chama hicho.

Juhudi za kumpata Katibu Mkuu wa Chama hicho Dr. Wilbroad Slaa ili kuzungumzia mgogoro uliopo ndani ya chama hicho katika Manispaa ya Musoma ambapo simu yake iliita bila kupokelewa.

Viongozi wa Chadema Musoma wanadai kuwa viongozi hao waliosimamishwa wamekuwa wakimpigia simu kumueleza mambo ya uongo. 


MWISHO
Read More...

Tuesday, February 19, 2013

MUSOMA YAPITISHA BAJETI YA SH. BILIONI 19, MWAKA 2013/14

 Wakuu wa Idara mbalimbali wa Manispaa ya Musoma wakisikiliza bajeti ya Mwaka 2013/14 kwenye kikao cha Madiwani kilichofanyika Februari 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo.
 Madiwani wa Manispaa ya Musoma wakisikiliza Bajeti ya Fedha ya mwaka 2013/14 ambayo ilisomwa na mchumi wa Manispaa hiyo John Masero kisha kuipitisha.
Diwani wa Kamnyonge Angela Derrick akitoa hoja juu ya ujenzi wa Barabara ya Biafra iliyopo kwenye Kata yake iliyotengewa kiasi cha Milioni 7 hivyo kuomba iongezwe ili kazi ifanyike kwa ufanisi mkubwa na kumaliza tatizo la barabara hiyo.




Na Thomas Dominick,
Musoma

MANISPAA ya Musoma imepitisha bajeti ya fedha ya mwaka 2013/14 Manispaa hiyo inatarajia kupata jumla ya shilingi Bilioni 19.751 ambayo imewekwa katika vipaumbele muhimu vitano.

Akisoma bajeti hiyo juzi Mchumi wa Manispaa hiyo, John Masero alisema kuwa vipaumbele hivyo ni pamoja na kuboresha elimu ya msingi na sekondari kwa kuhakikisha tatizo la upungufu wa madawati linatatuliwa na kuendelea kujenga matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na maabara.

“Pamoja na hayo juu vipaumbele vingine ni pamoja na Kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na vyanzo vyetu wenyewe, kuboresha huduma za kiuchumi kwa kukarabati barabara za manispaa na masoko, kuporesha huduma za afya kwa kuongeza ufanisi na upanuzi wa huduma,”alisema Masero.

Vipaumbele kingine ni kuimarisha uhusiano na wadau mbalimbali wa maendeleo pamoja na kutafuta wadau wengine wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kuendeleza manispaa hiyo ya Musoma.

“Mheshimiwa Mwenyekiti katika kipindi cha fedha 2013/14 Manispaa yetu inatarajia kupata jumla ya shilingi Bilioni 19.751 ilinganishwa na Bilioni 29.101 zilizokisiwi kwa kipindi cha mwaka 2012/13 ikiwa ni upungufu wa Bilioni 9.350 upungufu huu umetokana na upungufu wa fedha za miradi ya maendeleo,”alisema.

Masero alifafanua kuwa fedha hizo zitapatikana katika mapato ya Halmashauri ambayo yatakuwa ni Bilioni 1.615 na Bilioni 18.135 kutoka serikali kuu na wadau wengine. Ambapo Halmashauri hiyo  itapata mapato kutoka vyanzo vya kodi mbalimbali, ushuru wa huduma, leseni mbalimbali, leseni za pombe, karo za wanafunzi shule za sekondari na mapato mengine.

Kwa upande wa matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 Manispaa hiyo imekisia kutumia Bilioni 12.111 kwa mishahara ambapo halmashauri hiyo ina watumishi 1,477 walioko katika idara za utawala, fedha, elimu ya msingi, elimu ya sekondari, mipango na uchumi, afya, ujenzi, mipango miji, maendeleo ya jamii, kilimo na mifugo pia mwaka 2013/14 inatarajia kuajiri watumisha wapya 207.

Baada ya kumaliza kusoma bajeti hiyo madiwani wa Manispaa hiyo waliijadili kasha kuipitisha kwa pamoja na Diwani wa kamnyonge Angela Derrick alilalamikia kutengewa fedha kidogo kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Biafra yenye urefu wa kilomita 1 ambayo imetengewa shilingi milioni  7 ukilinganisha na kata zingine zenye barabara za kilomita 2 zimetengewa shilingi milioni 20.

“Mheshimiwa mwenyekiti inasikitisha kuona kuwa Kata yangu imetengewa shilingi milioni 7 kwa barabara yenye urefu wa kilomita 1 wakati Kata zingine zenye barabara zenye urefu wa kilomita 2 wamepewa shilingi milioni 20 hapa hakuna usawa tugawane wote sawa hata kama kasungura kikiwa kadogo,”alisema Angela.

Ambapo mchumi huyo alisema kuwa fedha za ujenzi wa barabara zinaombwa kila mwaka mwaka hivyo zitajadiliwa tena mwaka wa fedha ujao ili kumaliza tatizo la mtaa wa Biafra na sio kugombania fito wakati wanajenga nyumba moja.

Mwisho Meya wa Manispaa hiyo Alex Kisurura aliwaomba madiwani kuwaelimisha umuhimu wa kulipa kodi na fedha zitakazopelekwa kwenye kata zao zifanye kazi za maendeleo ili wananchi waone faida ya kodi zao.

“Usimamizi wa fedha wa fedha za miradi uwe mzuri na kuwashirikisha wananchi kwenye maamuzi pia wananchi nao walinde miradi hiyo”, alisema Kisurura.

Kabla ya bajeti hiyo kupitishwa madiwani wa Manispaa hiyo walilazimika kuitisha kikao cha dharura kilichofanyika Februari 16 mwaka huu kujua nani alipitisha bajeti hiyo ambayo ilipelekwa waizarani Januari 31 mwaka huu bila kupitia kwenye kamati mbalimbali za Manispaa kasha baraza la madiwani.

Hali hiyo iliyopelekea Meya kukalia kuti kavu hadi Mkurugenzi Ahmed Sawa alipotoa ufafanuzi wa kutosha ambapo aliwaambia hali hiyo ilitokana na mabadiliko ya Bunge la bajeti litakalofanyika mwezi Aprili mwaka huu. 

Mwisho
Read More...

Monday, February 18, 2013

MEYA WA MANISPAA YA MUSOMA ANUSURIKA KUNG'OLEWA KATIKA MADARAKA YAKE.




 *Mwisho baada ya kuona imeshindikana wakatoboa siri 
* wasema mtego huo ulikuwa haumuachi madarakani
 *Mwenyekiti wa Chadema Mkoa ajikanyanga kwenye maelezo yake


 Diwani wa Kata ya Baruti Swaibu Mohamed (CCM) akitoa hoja kuhusiana kwa ukiukwaji kwa taratibu za kuwasilisha Bajeti ya Manispa ya Musoma ya Mwaka 2013/14, Bajeti hiyo iliwasilishwa Wizara ya Fedha bila kukaa kwa kamati za Manispaa hiyo kisha kupitishwa kwenye Kikao cha Madiwani.

 Diwani wa Kigera (CUF) Gabriel Ocharo akimbana Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa madai ya ukiukwaji kwa taratibu za kuwasilisha Bajeti ya Manispa ya Musoma ya Mwaka 2013/14, Bajeti hiyo iliwasilishwa Wizara ya Fedha bila kukaa kwa kamati za Manispaa hiyo kisha kupitishwa kwenye Kikao cha Madiwani. 

 Angela Derrick Diwani wa Kata ya kamnyonge (CHADEMA) akieleza masikitiko yake yaliyofanywa na watendaji wa Manispaa ya Musoma kwa ukiukwaji kwa taratibu za kuwasilisha Bajeti ya Manispa ya Musoma ya Mwaka 2013/14, Bajeti hiyo iliwasilishwa Wizara ya Fedha bila kukaa kwa kamati za Manispaa hiyo kisha kupitishwa kwenye Kikao cha Madiwani. 

 Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Ahmed Sawa akisoma na kutolea ufafanuzi wa kina uliosaidia kumnasua Meya wa Manispaa hiyo Alex Kisurura kung'olewa kwenye madaraka yake, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa  waliamua kupeleka Bajeti ya Manispaa hiyo bila kupitia kwenye kamati husika kisha kwenye baraza la Madiwani ambapo madai yake makubwa yalikuwa ni kutokana na kubadilika kwa ratiba ya Bunge la bajeti ambalo litakaa Aprili mwaka huu badala ya Juni.



                                         Nyie wote ni mabwana wadogo hamuwezi kuning'oa ng'o!
 Mstahiki Meya wa Manispaa ya Musoma Akitoa maelezo yake baada ya kuona ameelemewa na madiwani kuhusiana na habari kuwa amehusika kusaini na kupeleka Bajeti ya Manispaa hiyo bila kufuata taratibu za kupitia kwanza kwenye Kamati za Manispa kisha kwenye baraza la madiwani.

Na Thomas Dominick
Musoma

MEYA wa Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara Alex Kisurura (Chadema) amenusurika katika mtego wa kung’olewa madarakani baada ya madiwani wa Manispaa hiyo kuitisha Baraza la dharura ili kujua kwa nini Rasimu ya Bajeti ya mwaka 2013/14 ilipelekwa hazina bila kufuata taratibu za Manispaa hiyo inayoongozwa na Chadema.

Kikao hicho kilichokaa mwishoni mwa wiki kuanzia saa 8 mchana hadi saa 11 jioni kilikuwa mikakati hiyo ilianza hivi karibuni baada ya kumtuhumu kuwa alishirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa Ahmed Sawa kuwa wamepitisha na kusaini bajeti hiyo bila kufuata taratibu.

Mpango huo ulianza kuonekana baada ya wajumbe wa kamati mbalimbali kugoma kwenda kwenye vikao vya kutipia bajeti wakidai kuwa hawawezi kukaa hadi watakapoambia ni utaratibu gani umetumika kupitisha bajeti hiyo.

“Bajeti yetu lazima iwe ya uwazi na ilitakiwa ijadiliwe na kamati
mbalimbali kisha kuletwa kwenye kikao cha madiwani ili tuweze
kuipitisha kisha kwenda wizarani, sasa tunataka kujua ni taratibu gani zimepelekea bajeti hiyo kufika wizara ya fedha bila sisi madiwani kuja? Alihoji Angela Derrick Diwani wa Kamnyonge.

Baada ya vuta nikuvute ya hapa na pale huku Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Sawa alitoa maelezo ya kina kwa kusema kuwa Serikali ilitoa maelekezo kuwa bajeti ya mwaka 2013/14 ilitakiwa kuwasilishwa Wizara ya fedha haraka iwezekanavyo kabla ya Januari 31 mwaka huu.

“Baada ya kupokea barua kuwa inatakiwa bajeti ya mwaka 2013/14 na muda uliobakia ni mdogo ilibidi tufanye haraka kukimbizana na muda na hii imetokana na mabadiliko ya kikao cha Bunge la bajeti ambalo litakaa mwezi Aprili mwaka huu,”alisema Sawa.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa baada ya kuifikisha bajeti hiyo wizarani waliiomba wizara ya fedha kuwa hiyo iliyopelekwa sio bajeti kamili bali ni rasmu kutokana na kutopita kwenye kamati za Manispaa husika na kuomba kuwa bajeti kamili itapelekwa baada ya kukaa na kujadiliwa na kamati husika.

Alisema kuwa bajeti kamili inatakiwa kufikishwa hazina Februari 20 mwaka huu ambapo mkurugenzi huyo aliitisha vikao vya kamati mbalimbali lakini wajume  wake waligomea kuhudhuria vikao husika hadi watakapopata majibu ya kina.


Kutokana na maelezo marefu ya Mkurugenzi huyo madiwani walianza kuhoji kuwa nani aliyesaini bajeti ambapo hapo ndipo walipokuwa wanasubiria kuona kuwa Meya Kisurura kama amehusika kusaini ili mtego wao wa kumtimua utimie.

Baada ya kuzungusha huku na kule ndipo Diwani  Zeddy Sondobi akaamua kutoboa siri iliyojificha nyuma ya panzia kuwa ulikuwa umetegwa mtego ambao kama angehusika kusaini bajeti hiyo ukomo wa Umeya wake ungekuwa vumefika.

“Kwanza taarifa ya Meya ilikuwa inatuchanganya kuwa halmashauri zingine zilikaa kabla ya bajeti hiyo kupelekwa wizarani na tukawa tunaulizana bajeti yetu imeendaje bila kusainiwa tukajua lazima utakuwa umesaini na mtego wetu huu safari hii usingeruka,”alisema Sondobi Diwani wa Bweri.

Baada ya kikao hicho mwandishi wa Blog hii alimtafuta mwenyekiti wa Chadema Mkoa, Charles Kayele na kufanya naye mahojiano kuwa chama hicho kilifanya kikao cha siri ili kujadili suala hilo na kufikia maamuzi kuwa kama atakuwa ameshiriki kisiri kusaini bajeti hiyo ataondolewa nafasi hiyo.

“Hatukufanya kikao chochote kile ndani ya chama lakini tulikutana leo hii kabla ya kikao cha madiwani ambapo tulijadili sula hili na
kumuuliza meya kama ameshiriki katika kusaini bajeti hiyo ambapo
alikiri kuwa hakuusika na  wakati wa bajeti hiyo inaandaliwa alikuwa safirini Dar es salaam,”alisema Kayele.

Chama cha Demokrasia na Maendeo (CHADEMA) Manispaa ya musoma kimekuwa na mpasuko ndani ya chama hicho na migogoro ya hapa na pale ambapo wakati wameingia katika uchaguzi wa naibu Meya madiwani hao waliafikiana nafasi hiyo wampatie diwani wa CCM, ambapo mbunge wa  jimbo hilo Vicent Nyerere aliingilia kati na kumaliza tofauti hizo.

MWISHO

Read More...

Wednesday, February 13, 2013

WATU SITA WAFA MKOANI MARA KWA MATUKIO MBALIMBALI

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Japhet Lusingu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) akitoa taari za matukio yaliyotokea Mkoani humo baada ya watu sita kufariki dunia kwa matukio mbalimbali.



Na Thomas Dominick,
Mara

Watu sita wamekufa katika matukio mbalimbali Mkoani Mara na wengine tisa wakijeruhiwa ambapo Wanawake watatu wamekufa baada ya kupigwa na waume zao.

Katika matukio hayo ni mauaji wanawake watatu waliouawa baada ya kupiga na waume zao akiwemo mmoja aliyepigwa kutokana na ugomvi wa Ndala (Kandambili).

Akizungumza na waandishi wa habari jana Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Japhet Lusingu alisema kuwa matukio hayo yametokea kati ya mwezi Januari na Februari mwaka huu.

Tukio la kwanza lilitokea Februari 10 mwaka huu saa 3:00 asubuhi katika kijiji cha Tonyo kata ya Busumwa, Wilaya ya Butiama , Mkoani humo baada ya mwanamke aliyetambulika kwa jina la Happyness Lucas (25), aliyepigwa na mume wake aliyejulikana kwa jina la Rugera John (27).

Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa ndala ( Kandambili) ambazo mume wa marehemu alikuwa amamnunulia mke mdogo, marehemu alipelekwa katika Hospitali ya Butiama kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini Februari 11 alifariki dunia.

Tukio jingine lilitokea Januari 28 Mwaka huu Wilayani Bunda, katika Mtaa wa Chiringe, Mtu mmoja Rhobi Lucas (24) fundi cherehani akiwa nyumbani kwake alifika mume wake aitwaye Masumbuko Khamis akiwa ameongozana na hawara yake Joyce Manumbu.

Inadaiwa kuwa baada ya kufika mume wake alianzisha ugomvi na kuanza kumshambulia mke wake kwa mateke huku akishirikiana na hawara yake. Baada ya ugomvi mwanamke huyo aliamua kuondoka nyumbani kwake na
kwenda nyumbani kwa wazazi wake siku hiyo hiyo na alikwenda kutoa taarifa ya kushambuliwa.

Kamanda Lusingu alisema kuwa Januari 30 mwaka huu  naye Masumbuko alifika Polisi na kutoa taarifa kuwa ameshambuliwa na mke wake na baada ya taarifa hiyo mke wake alikamatwa na Januari 31 alifikishwa mahakamani.

Alisema kuwa februari 9 mwaka huu mwanamke huyo alizidiwa na hali yake kuwa mbaya kutokana na kipigo alichopigwa na mume wake kwa kushirikiana na hawara yake na kupelekwa Hospitali ya DDH Bunda kwa
matibabu lakini Februari 11 alifariki dunia. Jeshi hilo linamshikilia mwanaume huyo kuhusiana na kifo hicho.

Tukio la tatu, lilitokea Februari 11, mwaka huu saa 1:30 asubuhi maeneo ya Kijiji cha Mkirira wilaya ya Butiama, mwanamke aliyejulikana kwa jina la Ziada Sasita (35) mkazi wa kijiji cha Kabegi aliuawa kwa kunyongwa shingo yake kwa kutumia nguo yake mtandio hadi kufa na watu wasiojulikana.

Marehemu alikuwa anatokea kwa mjomba yake maeneo ya mkirira ambako alikuwa ameenda kumsalimia na siku ya tukio alikuwa anarudi kabegi ambako alikuwa ameolewa. Mwili wa marehemu ulikutwa na mtandio shingoni na ulimi wake ukiwa umetoka nje.

Hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.

Tukio la nne lilitokea Februari 9 mwaka huu saa 9:00 jioni katika kijiji cha Nambubi Tarafa ya Nansimo wilayani Bunda Mkoani humo mwanamke aliyejulikana kwa jina la Edith Christopher (36) alishambuliwa kwa kupigwa na mpini wa mundu tumboni, mgongoni na kifuani na kufariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali.

Mtuhumiwa wa tukio hilo ni mume wa marehemu aitwaye Elephasi Maitabo (58) mtuhumiwa amekamatwa na polisi na atafikishwa mahakamani mara taratibu zitakapokamilika na chanzo cha mauaji hakijajulikana.

Tukio la tano,  ni la ajali ya mwendesha pikipiki kugonga kizuizi cha standi mpya ya mabasi wilayani Bunda ambapo mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Maka mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 20 akiwa na pikipiki ambayo haikuwa na namba ya usajili, chanzo cha tukio hilo ni mwendo kasi wa mwendesha pikipiki.

Tukio la mwisho ni lilitokea Februari 10 mwaka huu saa 4:15 usiku katika kijiji cha Msinganyi wilayani Bunda  ambapo gari aina ya Fuso lenye namba ya usajili T 677 BLQ mali ya Masunga Bugubugu mkazi wa Bariadi iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina lake hadi sasa.

Gari hiyo ilikuwa inatokea kijiji cha Kenyamonta wilaya ya Serengeti ambako kulikuwa na mnada iliacha njia njia na kupinduka na kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Magoti mwenye umri kati ya miaka 35 hadi 40 mdfanyabiashara mkazi wa makutano wilaya ya Butiama na wengine tisa kujeruhiwa.

Kamanda Lusingu aliwataja waliojeruhiwa ni Grace Masoka (40), Prisca Gwasi (42), Chausiku Mashara (35), Neema Hamis (25), Chacha Mwita (34), jamwela Wambura (30), Hassan Bunge (34), Juma Komba (22) na mary Rashid (37) wote wakazi wa Wilayani Bunda.

Kamanda Lusingu ametoa wito kwa wanaume wa Mkoa wa Mara kuacha kutumia nguvu na mabavu kwa wake zao kwani matukio ya aina hiyo yamezidi, pamoja na madereva wanaoendesha magari na pikipiki kuwa waangalifu
wanapoendesha vyombo hivyo ilikuepusha ajali zinazosababisha vifo na majeruhi.

MWISHO

 
Read More...